HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha Mkoani Pwani imetoa mikopo ya jumla ya shilingi milioni 991.5 kwa vikundi 51 vya ujasiriamali.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa wakati wa hafla ya utoaji mikopo ya robo ya tatu.
Shemwelekwa amesema kuwa fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 359 ni kwa vikundi 17 vya wanawake shilingi milioni 557 kwa vikundi 25 vya Vijana.
"Kiasi cha shilingi milioni 75.5 kilitolewa kwa watu wenye ulemavu 17 ambapo fedha hizo zimetokana na asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha,"amesema Shemwelekwa.
Amesema kuwa miradi iliyokopeshwa kwa vikundi hivyo ni pamoja na mradi wa usafirishaji ambapo pikipiki 25 zimetolewa na TOYO moja, Bajaji nne, pia miradi ya ufugaji kuku, uchomeleaji ,ushonaji na hardware.
"Viwanda vidogo vya utengenezaji batiki, sabuni, kilimo cha umwagiliaji, kiwanda na stationery miradi hiyo yote inatokana na vikundi hivyo ambavyo ni vya wajasiriamali,"amesema Shemwelekwa.
Aidha amesema kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 ambapo mikopo ilianza kutolewa mwezi Disemba 2024 kwa kanuni mpya hali ya urejeshaji kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu imefikia asilimia 52.
"Pia mikopo ya mwaka huu wa 2025/26 ambayo imetolewa kuanzia mwezi Novemba 2025 marejesho yamefikia asilimia 26 ambapo inaashiria marejesho yapo vizuri,"amesema Shemwelekwa.
Kwa upande wake Mgeni rasmi Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka amesema kuwa kutolewa mikopo hiyo ni jitihada kubwa zinazofanywa katika ukusanyaji wa mapato.
Koka amesema kuwa Halmashauri imeendelea kuimarika kwenye upande wa mapato hali ambayo inaongeza utoaji wa mikopo kutokana na asilimia 10 ya mapato.
Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha Lulu ya Wajane Kanyenda Mweri alisema kuwa fedha hizo zitawasaidia wao kama wajane kukuza mtaji wao wa ufugaji wa kuku.
Mweri alisema wanaishukuru Halmashauri na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha mikopo hiyo ya asilimia 10 baada ya kusitishwa kwa muda na kuwekwa utaratibu mpya.

No comments:
Post a Comment