Tuesday, June 9, 2026

LULU YA WAJANE KUANZISHA MRADI WA MINOFU YA KUKU

KIKUNDI cha Lulu ya Wajane kilichopo Kongowe Wilayani Kibaha Mkoani Pwani kinatarajia kuanzisha mradi wa uuzaji wa minofu ya kuku.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kikundi hicho Kanyenda Mweri wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kikundi hicho ambacho kinajihusisha na ufugaji wa kuku.

Mweri amesema kuwa kikundi chao kinaundwa na wanachama watano kiliwezeshwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha mkopo wa asilimia 10 kiasi cha shilingi milioni 46 ambapo tayari wameshazirejesha.

"Tumeomba mkopo mwingine wa fedha nyingi kidogo ambapo tutanunua mashine ya kuchakata minofu, mashine ya kunyonyolea kuku, mashine ya kutotolesha na kuuza vifaranga, mashine ya kusaga vyakula vya kuku na kufufua mashine ya kusaga unga,"amesema Mweri.

Amesema kuwa tayari wameshafanya utafiti juu ya soko la minofu ambapo mbali ya minofu watauza kuku na viungo vyake ikiwemo miguu, vichwa na vyote vitokanavyo na kuku.

"Uwezo wa kurejesha mkopo tutakaokopeshwa tunao kwani mkopo uliopita tulikopeshwa milioni 46 tukazirejesha mapema kabla ya muda kwani tulipewa miaka mitatu kurejesha lakini tulirejesha kwa miezi 11 tu na kupewa cheti cha wajasiriamali bora,"amesema Mweri.

Aidha amesema kuwa kutokana na mradi wa ufugaji kuku unaoendelea kila mwezi wanajilipa kiasi cha shilingi  100,000 pia wameweza kuwaajiri mabinti wa wawili ambao ni wahitimu wa vyuo wakiwa na diploma ya mifugo ambao ndiyo wanafanya shughuli za kitaalamu na kijana mmoja wa kiume.

"Tunamshukuru Mungu kwani ameweza kutuunganisha na kutupa mshikamano ambao ndiyo siri ya mafanikio yetu na ushirikiano tunaoupata kutoka kwa wataalamu wa Halmashauri na Mkurugenzi,"amesema Mweri..

Amesema kuwa walianzisha kikundi hicho kwa malengo ya kusaidiana kutatua changamoto na kutafuta fursa mbalimbali za ujasiriamali na kûwa na miradi ya kiuchumi endelevu kwani wanawake wanapofiwa na waume zao ndugu huwanyanyasa naa kuwanyanganya mali. 

"Matarajio yetu ni kuwa kikundi imara na hodari ambapo kwa sasa tayari wameanzisha kikundi cha vijana wanawake wanaojulikana kama Lulu Nazi wanaozalisha bidhaa zitokanazo na nazi,"amesema Mweri.

Ameongeza kuwa wanaiomba Halmashauri wawapatie mikopo kutokana na maombi kwani malengo wanakuwa wameshayaweka hivyo kuwakopesha chini ya walichoomba husababisha kufanya malengo yasifikiwe ya kile walichokiombea.

"Pia watoe mikopo kwa muda uliopangwa ambapo wao wanasubiri awamu ya pili tangu Desemba mwaka jana hadi leo bado hawajapata mkopo waliouomba ambapo gharama zinaongezeka za mahitaji mfano chakula cha kuku bei imeongezeka na mkopo hesabu zilizopigwa tayari zinakuwa chini,"amesema Mweri.

Amewataka wanawake wajane kutokata tamaa katika kupambania maisha yafamilia zao kwani wao ndiyo walezi wa familia na kulinda maadili ya watoto wao na kikundi hicho kilianzishwa mwaka 2022 na kimesajiliwa.

mwisho.







 



 

No comments:

Post a Comment