KIJANA mwenye wazo bora kati ya vijana 100 watakaowania kinyanganyiro cha Vijana Uchumi Challenge anatarajiwa kujinyakulia kitita cha shilingi milioni 50.
Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Dk Kedmon Mapana wakati akizungumza na vijana hao 100 watakaokuwa kambini kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha Mkoani Pwani.
Mapana amesema kuwa wapili akijinyakulia shilingi milioni 20 na watatu milioni 10 ambapo vijana wanaoshiriki ni wenye umri chini ya miaka 35 kutoka nchi nzima.
"Wizara ilitoa shindano la vijana kutoa wazo la kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia mawazo ya vijana kukuza ubunifu na Ujasiriamali na kuwapa vijana fursa ya kuonyesha mawazo yao ya kibiashara na miradi ya kibunifu inayoweza kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi,"amesema Mapana.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya Vijana Uchumi Challenge Joseph Malecela amesema kuwa jumla ya mawazo zaidi ya 7,000 ya vijana kote nchini yaliwasilishwa na kuchujwa na kubaki 100 ambayo yatashindanishwa kupata mshindi.
Malecela amesema kuwa washiriki hao 100 ambao wameingia kambini kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere watachujwa na majaji wabobezi wa masuala ya uchumi na fedha na kubaki 30 na baadaye 10.
Kilele kinatarajiwa kufanyika Jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

No comments:
Post a Comment