WALIPA kodi wa Mkoa wa Pwani wametakiwa kulipa kwa wakati ili kuonesha uzalendo kwa nchi na mapato yanayokusanywa yaweze kutumika kwenye miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo.
Hayo yalisemwa na Lilian Shirima aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kibaha wakati wa mazoezi ya wadau na walipakodi ikiwa ni kuelekea miaka 30 ya mamlaka hiyo.
Shirima alisema kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo inatokana na kodi zinazolipwa hivyo wanapaswa kulipa kodi kwa wakati ili zifanikishe malengo ya utekelezaji wa miradi hiyo.
"Wafanyabiashara wanapaswa kutoa risiti pale wanapofanya mauzo na wananchi nao wanapaswa kudai risiti pale wanaponunua bidhaa kwani huo ndiyo uzalendo wa nchi,"alisema Shirima.
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani Peter Eliona alisema kuwa wafanyabiashara wanapaswa kuwa na utamaduni wa kulipa kodi kwani kukwepa kulipa kodi ni kurudisha nyuma maendeleo ya nchi ambapo mapato hayo yanaleta maendeleo.
Eliona alisema kuwa kulipaji kodi ni uzalendo hivyo wanapaswa kulipa kodi kwani fedha zinazokusanywa kazi yake kubwa ni kuleta maendeleo kupitia miradi mbalimbali hasa ile mikubwa kama vile miradi ya elimu afya miundombinu ya barabara na reli.
Alisema kuwa fedha hizo matumizi yake ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wananchi hivyo kutolipa kodi na kurudisha nyuma jitihada za serikali za kuleta maendeleo kwa wananchi.
Aidha alisema kuwa katika kuelekea miaka 30 ya TRA wamefanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha afya kwa kufanya mazoezi kufanya usafi kwenye eneo la wafanyabiashara Chalinze.
"Ulipaji wa kodi unasaidia serikali katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi zikiwemo za kiafya na huduma zote ambazo wananchi wanapaswa kuzipata kwenye maeneo yao,"alisema Eliona.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara (JWT) Mkoa wa Pwani Abdala Ndauka alisema kuwa ulipaji kodi umekuwa rahisi kwa sasa kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo baiba ya wafanyabiashara na mamlaka.
Ndauka alisema mtaji mkubwa wa mfanyabiashara ni afya njema hivyo mazoezi hayo yanasaidia kuimarisha afya na kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

No comments:
Post a Comment