Monday, June 29, 2026

AKINAMAMA WATAKIWA KUWAKUMBUKA VIJANA WAKIUME

MWANASIASA mkongwe na aliyewahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Sophia Simba ameitaka jamii kuwawezesha kiuchumi vijana wa kiume ambao wamesahaulika.

Simba ameyasema hayo Mjini Kibaha wakati wa kuadhimisha miaka 10 ya Kikundi cha Super Women 2017 na kuwa baada ya wanawake kufanikiwa vijana wakiume nao waangaliwe.

Amesema kuwa kwa muda mrefu jamii iliwekeza kudai haki za wanawake ambapo kwa sasa wamepiga hatua ya kimaendekeo baada ya nguvu kubwa kutumika huku wale wa kiume wakiwa wamesahaulika.

Simba ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora alisema kuwa kwa sasa vijana wa kiume wana hali mbaya kiuchumi.

"Tumshukuru Mungu kwani kwa sasa wanawake angalau wamepiga hatua kiuchumi tuwaangalie na vijana wakiume ili nao kwa kuwajengea uwezo wa kiuchumi,"amesema Simba.

Aidha alikipongeza kikundi hicho kwa mafanikio waliyoyapata kwa muda huo tangu kuanzishwa kwake kwani baadhi ya vikundi vinaanzishwa na havichukui muda mrefu vinakufa.

Naye mwanzilishi wa kikundi hicho Beth Msimbe amesema kuwa wamepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kukopeshana fedha kwa riba nafuu kupitia mfuko wa kikundi kwa fedha wanazoweka ambapo mkopo ni mara tatu ya fedha waliojiwekea.

Msimbe amesema kuwa wameweza kukuza biashara zao na kuwa wafanyabiashara wakubwa pia wamekuwa wakifanya matendo ya huruma kwa watu wenye uhitaji na kuwataka wanawake wawe na wavumilivu kwa kufuata sheria na taratibu.

Kwa upande wake mwenyekiti kikundi hicho Betha Kimambo amesema kuwa wanatarajia kuanzisha mradi wa kukodisha vyombo ili kuongeza kipato ndani ya kikundi.

Kimambo amesema kuwa mbali ya kupata mafanikio kuna baadhi ya changamoto ikiwa ni pamoja na baadhi ya wanachama kujitoa.





No comments:

Post a Comment