Tuesday, June 23, 2026

PWANI YAKUSANYA BILIONI 266

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 266 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita na kuvuka malengo yaliyowekwa ya kukusanya shilingi bilioni 235 katika kipindi hicho.

 

Akizungumza kwenye Kongamano la Mamlaka hiyo ya kutimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Peter Jackson alisema kuwa mafanikio hayo ni ongezeko la asilimia 113 ya makusanyo kwa kipindi hicho.

 

Jackson alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano ulioonyeshwa na wafanyabiashara na wadau wote wa kodi ambapo katika kipindi hicho malaengo ya makusanyo yalikuwa ni bilioni 23 lakini zilikusanywa kiasi cha shilingi bilioni 27.

 

“Kwa wastani makusanyo kwa kipindi cha miaka 10 ni ongezeko la asilimia 10 ambapo yamekuwa yakiongezeka hadi kufikia kiasi hicho na kuonyesha jinsi gani mamlaka hiyo inavyopiga hatua katika kuleta maendeleo ya nchi,”alisema Jackson.

 

Alisema kuwa makusanyo yana faida kubwa kwani yanatumika kwa ajili ya kufanya shughuli za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ikiwemo ya barabara ujenzi wa reli ya kisasa SGR huduma za afya, huduma za elimu na masuala mbalimbali.

 

Aidha alisema kuwa ukusanyaji wa mapato makubwa ndiyo njia ya kukuza uchumi wa nchi ambapo walipa kodi wanapaswa kulipa kwa hiyari na kwa wakati ili kuondoa changamoto za kupewa adhabu ambayo inawarudisha nyuma.

 

“Kwa sasa tumeweka mifumo madhubuti ya ukusanyaji na namna ya kuwafikia kwa urahisi walipa kodi na kuwaondolea usumbufu wa kufika ofisini badala yake wanauwezo wa kulipa au kufanya shughuli zote wakiwa maeneo yao jambo ambalo limerahisisha utendaji kazi,”alisema Jackson.

 

Akizungumzia kuhusu changamoto alisema kuwa ukuaji wa uchumi usio rasmi umekuwa ni tatizo kwani unakuwa nje ya mfumo rasmi hivyo kusababisha kukosekana kwa mapato kutokana na kukwepa au kupunguza kodi kuongezeka kwa biashara mtandaoni biashara haramu na za magendo ambazo huathiri ushindani wa kibiashara..

 

Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mkoa wa Pwani Abdala Ndauka alisema kuwa baadhi ya wafanyabiashara hawana uelewa juu ya masuala ya ulipaji kodi hivyo kuna haja ya kutolewa elimu ya kutosha.

 

Ndauka alisema kuwa ulipaji kodi unapaswa kuwa rafiki na si kama adhabu bali uwe rafiki hata hivyo malalamiko kwa sasa yamepungua kwani kwa sasa kumekuwa na majadiliano juu ya changamoto zinazowakumba walipa kodi na watengeneze walipa kodi wapya.

 

Mwenyekiti wa Chemba ya wafanyabiashara Mkoa wa Pwani Said Mfinanga alisema kuwa matumizi ya teknolojia yamesaidia kuwapunguzia muda walipa kodi kwenda ofisini ili kufanya kufanya taratibu mbalimbali juu ya masuala ya ya biashara zao.

 

Mfinanga alisema kuwa mfumo wa teknolojia pia utumike kutoa elimu juu ya masuala ya ulipaji kodi na taratibu zote zihusikanazo na masula ya kodi ili kujenga uelewa wa pamoja kwa walipa kodi na mamlaka hiyo ambayo inajuhusisha na ukusanyaji wa mapato ya serikali.   

 

Naye mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) Mkoa wa Pwani Philemon Maliga alisema kuwa ili kuboresha ukusanyaji wa mapato Mamlaka inapaswa kuwa na mahusiano bora na mazuri na walipakodi kwnai kundi lao ni kubwa na lina uwezo wa kuchangia pato la serikali.

 

Maliga alisema kuwa TRA iatoe limu kuanzia mashuleni na sehemu mbalimbali ili kuwajengea walipa kodi utamaduni wa kulipa mapato ili kuonyesha uzalendo wa nchi yao kwani kodi ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo.

 

No comments:

Post a Comment