Tuesday, April 16, 2024

WANAOTUKANA VIONGOZI KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni amesema kuwa  wanaotumia mitandao kuwatukana viongozi wa nchi  watakumbana na mkono wa sheria popote walipo.

Masauni ametoa kauli hiyo Aprili 15/2024  katika kumbi wa habari Maelezo Jijini  Dodoma alipokuwa akijibu swali la mmoja wa waandishi wa habari aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kuwachukulia hatua watu wanaomtukana Rais Samia katika mitandao.

Amesema kuwa hawatakuwa na msamaha  kwa mtu yoyote atakayevunja sheria ya kutukana viongozi na atatafutwa popote mpaka apatikane.

‘’Mimi niseme tu Serikali haina msalie mtume kwa mtu yeyote anayevunja sheria kwa kutukana viongozi katika mitandao na ina mkono mrefu wanaofanya hivyo watatafutwa popote walipo mkono wa sheria utawakamata,’’amesema Masauni.

Aidha Masauni ambaye alikuwa akielezea mafanikio ya miaka 60 ya Muungano amesema tangu enzi za waasisi wa Muungano Mwalimu Nyerere na Amani Karume walijenga Taifa lenye maadili hivyo ni budi kuendeleza yale waliyoacha waasisi wetu.

Sambamba na hayo ametoa wito kwa wananchi kuwa Serikali haitamfumbia macho mtu au kikundi cha watu wanaotukana viongozi kupitia mitandao  kwa kuwachukulia hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine.

‘’Msifikirie haya mambo yanayoenendelea mitandaoni na kutukana watu hawachukuliwi hatua utajikuta na wewe unafuata mkumbo usiige kwani hakuna atakayeachwa salama,"amesema Masauni.

Waziri huyo amesema kuwa hatua kali zitachukuliwa kwani Serikali ya Rais Samia haipendi kusumbua watu inataka watu waishi kwa amani na kila mmoja atii sheria bila shuruti.

‘’Dhamira ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapendi kuona watoto wake wanapata shida hivyo vyombo vya usalama vipo kazini’’, amesema Masauni.

Pia amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano sekta ya usalama wa nchi  iko vizuri na mafanikio ni mengi ikiwemo kuwa na majeshi ya polisi imara.

No comments:

Post a Comment