Tuesday, April 16, 2024

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI YAONGEZA MELI ZA UVUVI BAHARI KUU

Na Wellu Mtaki, Dodoma

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu  (Deep Sea Fishing Authority-DSFA) imefanya maboresho katika kanuni za Sheria Uvuvi wa Bahari Kuu  na kupandisha utoaji wa vibali vya uvuvi katika Bahari Kuu kutoka  meli tisa mwaka 1988 hadi meli 61 mwaka 2023/24 kwa ajili ya kufanya uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari (EEZ) upande wa Tanzania.

Hayo yamesemwa Leo Tarehe 16 Aprili 2024 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Muungano kuelekea maadhimisho ya miaka 60.

Ameeleza kuwa DSFA imeingia mkataba na Kampuni ya Albacora ya nchini Hispania kwa ajili ya ujenzi wa  kiwanda cha kuchakata samaki katika Mkoa wa Tanga na kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 20 za samaki kwa siku, kuhifadhi tani 2,400 za samaki na kuajiri wafanyakazi zaidi ya 100.

Pia amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanga kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kukitumia Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Machui – Tanga kupata vifaranga vya samaki na viumbe maji wengine wakiwemo jongoo bahari kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa buluu.

Aidha, zaidi ya wananchi milioni 4.5 wanakadiriwa kupata kipato chao cha kila siku kutokana na shughuli za Uvuvi, zikiwemo kuunda na kutengeneza boti, kushona nyavu, biashara ya samaki na mazao yake pamoja na Baba na Mama lishe. 

Ikumbukwe kuwa sekta ya uvuvi ni miongoni mwa sekta tatu za Kilimo ambazo zinaajiri wananchi wengi na imeweza kutoa ajira za moja kwa moja kwa wavuvi 198,475 na wakuzaji viumbe maji wapatao 35,986.

No comments:

Post a Comment