Saturday, April 6, 2024

MTAA WA KWAMFIPA WAANZA UJENZI WA SEKONDARI

MTAA wa Kwamfipa Kata ya Kibaha Mkoani Pwani umeishukuru serikali kwa kuwapatia kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ambayo utawapunguzia changamoto wanafunzi wa Mtaa huo wanaotembea umbali wa Kilometa nane kwenda Shule ya Sekondari ya Simbani.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kibaha Mohamed Muanda alipotembelea kuangalia maendeleo ya ujenzi huo kwani ni ukombozi kwa wanafunzi wanaotoka kwenye Mtaa huo.

Muanda amesema kuwa hicho kilikuwa kilio cha wananchi wa Mtaa huo pamoja na Mtaa wa Mwendapole ambapo Mitaa hiyo miwili ina jumla ya shule tatu za Msingi ambapo wanafunzi wote husoma Shule hiyo ya Simbani ambayo ni ya Kata.

Kwa upande wake Mjumbe wa Serikali ya Mtaa huo Jumanne Mwinshehe amesema kuwa wananchi walijitolea kwa kufanya usafi kabla ya ujenzi kuanza huo ukiwa ni mchango wa wananchi na wataangalia fedha za Halmashauri zitaishia wapi ili wananchi wachangie ambapo ujenzi huo uko hatua ya msingi.

Naye Christina Sabai wanafunzi wanakwenda Sekondari mbali na kwa watoto wa kike ambao hukumbana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kurubuniwa na waendesha pikipiki na kuhatarisha masomo yao kwa kupata ujauzito.

Aidha fundi wa ujenzi wa mradi huo wa Shule hiyo Juma Mabula amesema watatumia siku 75 kukamilisha ujenzi huo kwani vifaa vyote viko hivyo wanaamini watakamilisha kwa muda uliopangwa ili wanafunzi waanze kusoma.

No comments:

Post a Comment