SERIKALI imetoa shilingi bilioni 696.7 kwa ajili ya kupunguza na kuondoa umaskini kwa kaya milioni 1.3 kwenye vijiji na mitaa.
Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya wizara hiyo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano.
Simbachawene amesema kuwa lengo la Serikali ya awamu ya sita na awamu zilizopita zinazoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kupunguza na kuondoa umaskini wa kipato.
Amesema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulianzishwa na serikali mwaka 2000 kama mojawapo ya mikakati ya kupambana na umaskini kwa kutumia dhana ya ushirikishaji jamii.
"Jumla ya miradi 1,704 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 72 ilitekelezwa kupitia mpango huu wa TASAF awamu ya I awamu hii ilitekelezwa kwa mafanikio makubwa katika kuwapatia wananchi huduma muhimu za kijamii katika sekta mbalimbali zikiwemo za maji, elimu, miundombinu na afya,”amesema Simbachawene.
Simbachawene amesema awamu ya Pili ya TASAF ilianza utekelezaji mwaka 2005 hadi 2013 katika Halmashauri zote za Tanzania Bara na wilaya zote za Tanzania Zanzibar.
Amefafanua kuwa jumla ya miradi 12,347 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 430 ilitekelezwa wakati wa Awamu hii ya Pili ya TASAF (TASAF II).
Amesema katika miaka 60 ya Muungano, serikali inayoongozwa na Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa ili wananchi waweze kupata huduma bora.
Aidha amesema kuwa TAKUKURU kwa kutambua kuwa Skauti ni suala la Muungano kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) ziumeunda timu ya uratibu ya kitaifa yenye Wajumbe kutoka Chama cha Skauti Tanzania (CST), ZAECA na TAKUKURU ili kuimarisha ushirikiano katika jitihada za kupambana na rushwa.
Pia amesema Ushirikiano huu ni muhimu sana kwa ustawi wa Taifa kwa kuwa Skauti wapo katika kundi la vijana na ni “Jeshi kubwa” ambalo tumeshuhudia likitoa mchango chanya katika matukio mbalimbali ya kijamii na kitaifa.
No comments:
Post a Comment