Saturday, April 27, 2024

WAWILI MATATANI KUMDHALILISHA DK KAWAMBWA

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata watuhumiwa wawili Hassan Usinga au Wembe na Abdallah Mgeni kwa tuhuma za kumdhalilisha aliyewahi kuwa Waziri wa Miundombinu Dk Shukuru Kawambwa.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamtaka mtu aliyechukua na kusambaza video hiyo mitandaoni ajisalimishe kituo cha Polisi Bagamoyo
mara moja.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani (SACP) Pius Lutumo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 24 saa 8 mchana huko Kitopeni Wilaya ya Bagamoyo.

Lutumo alisema kuwa tukio hilo lilionekana kupitia mitandao ya kijamii ambapo video ilionekana ikimwonyesha Waziri na Mbunge mstaafu Dk Shukuru Jumanne Kawambwa akishambuliwa kwa maneno makali na kudhalilishwa kwa kufokewa na
kutishiwa kufungwa pingu kama mhalifu na watuhumiwa hao hali ambayo iliyosababisha taharuki kubwa kwa jamii.

"Video hiyo ilionyesha Dk Shukuru Jumanne Kawambwa na mtu mwingine aitwaye Cathbert Enock Madondola walishambuliwa ambapo watuhumiwa hao baadae walipewa dhamana kwa mujibu wa sheria na watafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika,"alisema Lutumo.

Alisema kuwa Wembe alifanya tukio hilo akiwa na askari mgambo aitwaye Abdala Mgeni ambapo chanzo cha tukio hilo ni magari ya mchanga ya mtuhumiwa kuharibu barabara na mashamba.

"Mtuhumiwa alifikia hatua hiyo baada ya magari yaliyokuwa yakienda kuchukua mchanga kwa mbali ya kuharibu barabara wakati yakipita kwenda kubeba mchanga eneo hilo hali iliyosababisha wananchi kufunga barabara kwa magogo ili kuzuia uharibifu huo wa barabara,"alisema Lutumo.

Kamanda Lutumo alisema kuwa Dk Kawambwa ni moja ya  wakazi wa eneo hilo ambapo walijaribu kuyazuia magari hayo ili kupunguza uharibifu.

No comments:

Post a Comment