Na Wellu Mtaki, Dodoma
Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa Mfumo mpya wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma unaojulikana kama National e-Procurement System of Tanzania (NeST) kabla ya uwekezaji huu.
Ununuzi wa umma ulikuwa ukifanyika kwa kutumia mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma uliojulikana kama Tanzania National e-Procurement System (TANePS) ambao ulijengwa na kampuni ya kigeni kutoka Ugiriki lakini Serikali ilibaini changamoto nyingi kwenye ununuzi uliokuwa ukifanyika kupitia mfumo wa TANePS ikiwemo taarifa zote za Ununuzi wa umma kuwa chini ya usimamizi wa kampuni ya kigeni nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa kujenga uwezo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Amin Mcharo wakati akizungumza na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Jijini Dodoma, kuhusu mafanikio makubwa waliyopata katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa changamoto hii na nyinginezo zilipelekea uamuzi wa kuanzisha mfumo mbadala ambao utakuwa bora zaidi, wenye kuleta tija, unaojengwa na wataalam wa ndani na kusimamiwa na Serikali.
Aidha amewaasa wananchi kujisajili katika mfumoNeST na kuomba zabuni mbalimbali zinazotangazwa na Serikali ili kuweza kujipatia kazi na kuhakikisha anayeomba amekidhi vigezo vinavyotakiwa katika kuomba zabuni husika na pindi wanapopata zabuni wazifanye kwa uadilifu na ufanisi ili waendelee kuaminiwa katika miradi mingine kutokana zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya Serikali inatumika kwenye ununuzi wa umma.
Ikumbukwe kuwa PPRA imekuwa ikitekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kuwahudumia wananchi ili kutimiza lengo la Serikali iliyopo madarakani ya kupeleka huduma kwa wananchi na kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi na teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo, kama inavyoonyesha katika Sura ya kwanza,Kipengele cha 8(e) ya Ilani hiyo wakati sura hiyohiyo kipengele cha 8 (f) ikielezea kujikita katika kutengeneza ajira zisizopungua milioni 8 katika sekta rasmi na zisizo rasmi kwa ajili ya vijana.
No comments:
Post a Comment