Wednesday, April 24, 2024

PROFESA MKENDA ATAKA WATOTO WENYE CHANGAMOTO MAFURIKO WASAKWE WAENDE SHULE

WANAFUNZI ambao shule zao zimekumbwa na mafuriko nchini wataruhusiwa kusoma shule ambazo ziko jirani na wanakoishi ili wasikose masomo.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda alipotembelea kujionea hali halisi kwenye maeneo yenye taasisi za shule ambao zimekumbwa na mafuriko na kutoa misaada ya vifaa vya shule kwa baadhi ya Shule kwenye Wilaya ya Rufiji na Kibiti Mkoani Pwani.

Mkenda alisema kuwa wanafunzi ambao Shule zao zimekumbwa na mafuriko na hawataweza kusoma kutokana na mazingira hayo kuwa hatarishi na Shule kufungwa wanafunzi hao watasoma maeneo ambayo wazazi wao wamehamia ili wasikose elimu.

“Mfano tumejionea Shule ya Msingi Muhoro ili wanafunzi waende Shule inabidi wapande Mitumbwi kama sisi tulivyoapanda kiusalama siyo sawa kwani ni hatari kwa maisha yao na hata nyumba za walimu tumeona zimezingirwa na maji kwa hali hiyo ni vigumu Shule hiyo kuendelea kutumika hivyo wanafunzi hao wasome popote pale walipo ambapo ni jirani na wanapoishi kwani serikali haitaki mtoto akose elimu,”alisema Mkenda.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Caroline Nombo alisema kuwa wanaendelea kufuatilia maeneo yote nchini ambayo yanachangamoto za mafuriko ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma pia kutoa vifaa kwa wanafunzi na walimu ili kwa wale ambao vifaa vyao vimeharika na mafuriko wanapatiwa vingine ili masomo yaendelee.

Naye mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema kuwa wamechukua jitihada mbalimbali za kukabili changamoto hiyo ya mafuriko ambapo kwenye Shule ya Msingi Muhoro wameifunga Shule hiyo na nyingine na kuruhusu wanafunzi  kusoma kwenye Shule ambazo wako jirani nazo na hazina changamoto ya mafuriko.

Naye Ofisa Elimu Mkoa wa Pwani Sara Mlaki alisema kuwa Shule zilizoathirika na mafuriko Wilaya ya Rufiji ni 11 zenye wanafunzi 7,264 wasichana wakiwa ni 3,657 na wavulana 3,607 walimu 58 ambao nyumba zao zimeathirika.

No comments:

Post a Comment