SHIRIKA la Tanzania Health Promotion Support (THPS) limetoa msaada wa vifaa vya shule na vyakula kwa wahanga wa mafuriko katika Wilaya za Rufiji na Kibiti Mkoani Pwani.
Misaada hiyo ilikabidhiwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Bodi Profesa Mohamed Janabi ambaye amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa (THPS) Dk. Redempta Mbatia, viongozi kutoka Serikali za Mkoa wa Pwani na Wilaya za Rufiji na Kibiti, wahudumu wa afya, maofisa wa THPS na wananchi wenye mapenzi mema.
Prof Janabi amesema msaada huo wenye thamani ya Shilingi milioni 18.8 ni pamoja na vifaa vya shule zikiweno sare za shule, mabegi, madaftari na kalamu vyenye thamani ya shilingi milioni 7.8 huku kwa upande wa vyakula ni pamoja na unga wa mahindi kilo 1,500, maharage kilo 750 na mafuta ya kupikia dazeni 29.5 vyote vikiwa na thamani ya Shilingi milioni 10.9.
Amesema kuwa mahitaji hayo yanatarajiwa kutoa ahueni kwa waathirika wa mafuriko wakati wakijpanga kurejea kwenye shughuli zao mbalimbali za kiuchumi.
"THPS na wao kama moja wapo ya wadau wakubwa wa afya wanaofanya kazi mkoani Pwani tumeungana na Serikali katika jitihada za kusaidia watu waliokumbwa na mafuriko,"amesema Prof Janabi.
Aidha amesema kuwa wanatumai msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza adha wanayoipata wakazi wa Wilaya za Rufiji na Kibiti waliokumbwa na mafuriko.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge alitoa shukrani zake kwa THPS kwa msaada huo na kusema kuwa anatarajia kuendelea kushirikiana na Shirika hilo.
Kunenge amesema kuwa msaada huo utasaidia kuleta matumaini kwa watu waliopoteza mali na makazi kutokana na mafuriko hayo.
THPS ni Shirika lisilo la kiserikali lililoanzishwa mwaka 2011 na kupitia uimarishaji wa mifumo ya afya na jami linalenga katika kushughulikia changamoto mbalimbali za afya ya umma, ikiwa ni pamoja na VVU na UKIMWI, kifua kikuu, ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, huduma za afya ya uzazi, watoto wachanga, watoto nã vijana, maabara na mifumo ya taarifa za usimamizi wa afva, UVIKO- 19 na tathmini za afya ya umma.
No comments:
Post a Comment