Friday, April 19, 2024

KUNDI LA KIBAHA HURU FIKRA HURU LATOA MADAWATI 30

KUNDI la Whatsapp la Kibaha Huru Fikra Huru limetoa msaada wa madawati 30yenye thamani ya shilingi milioni tatu ili kusaidia wanafunzi ambao wanakabilia na upungufu wa madawati kwenye Shule za Msingi za Halmashauri ya Mji Kibaha.

Mwenyekiti wa Kundi hilo la Kijamii Mchungaji Paschal Mnemwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha mara baada ya kukabidhi madawati hayo amesema wameguswa na changamoto ya wanafunzi hao kukaa chini.

Mch Mnemwa amesema kuwa wameamua kuchangia madawati hayo ili kuisaidia serikali ili kukabiliana na changamoto hiyo ili wanafunzi wasome katika mazingira mazuri.

"Nawashukuru wana kikundi na watu mbalimbali kwa kutoa fedha na huu siyo mwisho kwani huo ni mwanzo wa kusaidia kumfuta vumbi mtoto wa Kibaha ili kumfanya mtoto awe na moyo wa kusoma na wadau mbalimbali wajitoe kusaidia tujenge tabia kusaidia maendeleo,"amesema Mnemwa. 

Amesema jamii isitegemee misaada toka nje bali ianze kuchanga yenyewe ili kusaidiana wenyewe kwa wenyewe badala ya kusubiri kusaidia kutoka nje ya nchi wafadhili wa kwanza iwe jamii yenyewe ili kuleta maendeleo.

"Mifumo ya mitandao ya kijamii ilitengenezwa ili kuiweka jamii pamoja kusaidiana na wasiitumie vibaya kwani endapo itatumika vibaya itaharibu maadili ya jamii ikitumika vizuri inaweza kuleta maendeleo,"amesema Mnemwa.

Akipokea madawati hayo mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mussa Ndomba amesema kuwa anawashukuru na kuwapongeza kundi hilo kwa kuunga mkono jitihada za serikali kwa kujitolea madawati hayo.

Ndomba amesema kuwa madawati hayo yatasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati kwenye shule mbalimbali za Mji wa Kibaha na kuwataka wadau wengine kuchangia kama walivyofanya kundi hilo.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Msingi Taaluma wa Halmashauri ya Mji Kibaha Adinani Livamba amesema kuwa wana upungufu wa madawati zaidi ya 3,000 ambapo madawati ni hitaji kubwa kwani wanafunzi wanafunzi wanaongezeka pia yanaharibika hivyo changamoto hiyo haiwezi kwisha kabisa.

Livamba amesema kuwa wanachukua hatua mbalimbali kukabili changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati wa madawati 1,321 na wanafanya na matengenezo na madawati hayo yatasaidia wanafunzi 90 wa darasa la kwanza, la pili na la tatu ambao ndiyo watanufaika.

Naye msemaji wa kundi hilo Hamis Mponji amesema kuwa fedha zimechangwa na watu wa Kibaha na nje ya Kibaha ambapo kulikuwa hakuna kiwango maalum cha kuchanga ni kile ambacho mtu kaguswa kukitoa.

Moja ya viongozi wa kundi hilo Hamad Kibwelele amesema kuwa wakati wanaanzisha kundi wakaona lisiwe na maongezi tu bali wafanye kitu cha maendeleo kwenye jamii na kukubaliana kuchangia madawati huku wakiangalia nini cha kufanya kwa baadaye ili kuleta maendeleo Kibaha.

No comments:

Post a Comment