MKURUGENZI wa Kampuni ya Njuweni Ltd Alhaj Yusuph Mfinanga ameahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni tano kwa mwanafunzi atakayefaulu na kuongoza kitaifa kwenye mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kutoka shule tatu zinazomilikiwa na kampuni hiyo.
Aidha atawasomesha bure wanafunzi 20 watakaofaulu masomo ya kumaliza elimu ya msingi na kupata alama za daraja A kwa masomo yote ambapo watasoma kwenye shule za sekondari za kampuni hiyo za Vuchama Islamic Secondary School na Mangio Secondary School zilizopo Mkoani Kilimanjaro.
Mfinanga ameyasema hayo wakati wa mahafali ya shule hizo ambazo ni Kibaha Independence School (KIPS), Anex na Msangani zote zilizopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.
Amesema kuwa ametoa fursa hiyo kama motisha kwa wanafunzi wa shule hizo ili kuhamasisha wafanye vizuri kwenye mitihani yao na kuzifanya shule hizo ziwe na matokeo mazuri.
Kwa upande wake mgeni rasmi Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka amesema kuwa sekta binafsi kwenye sekta ya elimu ina mchango mkubwa sana kwani inaipunguzia serikali mzigo wa wanafunzi.
Koka amesema kuwa licha ya ujenzi wa madarasa kujengwa na serikali mara kwa mara lakini bado kuna changamoto kubwa ya upungufu wa madarasa na miundombinu mingine hivyo ushirikiano na sekta binafsi unahitajika.
Kwa upande wake meneja wa KIPS Nuru Mfinanga amesema kuwa wanashirikiana vizuri na serikali katika kukabiana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwenye sekta hiyo lengo likiwa ni kutoa elimu bora.
Mfinanga amesema kuwa wanaipunguzia mzigo serikali kwa kuwasomesha wanafunzi kupitia sekta binafsi na kuwataka wazazi kuwafuatilia watoto wao ili wafanye vizuri kwenye masomo yao na kuwataka walipe ada kwa wakati ili waweze kujiendesha na kutoa elimu bora.
No comments:
Post a Comment