Wednesday, September 6, 2023

JAMII YAFUNDISHWA USAWA WA KIJINSIA KULETA MAENDELEO JUMUISHI


HALMASHAURI ya Mji Kibaha imedhamiria kuhakikisha inafikia asilimia 50 ya usawa wa kijinsia ili kuleta maendeleo jumuishi kwa wananchi.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na ofisa maendeleo ya jamii kitengo cha jinsia wa Halmashauri ya Mji Kibaha Maria Nkangali wakati wa mafunzo kwa watu maarufu kwenye jamii kupitia mradi wa uongozi wa wanawake na haki za kiuchumi (WLER).

Nkangali alisema kuwa hadi sasa wamefikia asilimia 20 kwenye mradi huo wa miaka mitano kuanzia 2021 hadi 2026 ambapo hadi sasa wako kwenye kata tatu za Visiga, Mkuza na Pangani.

"Lengo la mradi huu ni kuwa na usawa wa kijinsia kwenye masuala mbalimbali ikiwemo uongozi, uchumi, umiliki wa ardhi na kupata huduma za kijamii,"alisema Nkangali.

Kwa upande wake wakili wa serikali kutoka Halmashauri ya Mji Kibaha Elizabeth Lukumay  alisema kuwa baadhi ya ndoa zinakuwa ni batili kutokana na kutofuata taratibu za kisheria hivyo inapotokea zinavunjika mwanamke na watoto wanakosa haki.

Naye mwenyekiti wa wazee kata ya Mkuza Anangisye Mwakapande alisema kuwa changamoto za ndoa na ardhi ni kubwa sana kutokana na kutokuwa usawa wa kijinsia.



No comments:

Post a Comment