Thursday, September 7, 2023

JUMUIYA YA WAFANYABIASHARA TANZANIA WACHARUKA MKOANI MBEYA

 



WAFANYABIASHARA mkoani Mbeya waiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Mbeya kufanya marekebisho ya baadhi ya mifumo na Sheria za Kodi zinachochea rushwa .


Hayo yamesemwa na wafanyabiashara wa mkoani hapo wakati wa kupokea kero, maoni na changamoto za wafanyabiashara katika mkutano uliofanyika eneo la soko jipya la Mwanjelwa chini ya Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Hamis Livembe.

Wamesema kuwa TRA mkoani hapo imekuwa ikitumia mifumo hiyo kama chanzo cha mapato binafsi na si kuwasaidia kukuza biashara  za wafanyabiashara hao.

Aidha wameitaka serikali kutambua kuwa uchumi wa Watanzania wengi unajengwa kupitia biashara hivyo wanaiomba serikali ipunguze ututiri wa kodi .

Awali Mwenyekiti wa  Jumuiya wafanyabiashara Tanzania Hamis Livembe amesema kuwa moja ya sababu ya kufanya ziara mkoani hapo ni kukusanya changamoto , kero na maoni ili kuyatafutia ufumbuzi kwa mamlaka husika.

Livembe amesema kuwa zipo changamoto zinazowakumba wafanyabiashara hivyo kama kiongozi wa Jumuiya ya wafanyabiashara atahakikisha kero  zote zimetafutiwa ufumbuzi.

Naye katibu wa Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania Abdall Salim amesema kuwa wafanyabiashara wote Tanzania wanatakiwa kuungana kwa pamoja ili kukomboa biashara zao hivyo wanapaswa kujisajili na Jumuiya hiyo.

Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania ni Taasisi inayosimamiwa na wafanyabiashara wenyewe wenye lengo la kuhakikisha wanatatua changamoto za kibiashara.

No comments:

Post a Comment