Wednesday, September 27, 2023

WAFUGAJI KUTUMIA WALINZI SHIRIKISHI KULINDA MIFUGO YAO

KUFUATIA vitendo vya wizi wa mifugo kushamiri Chama cha Wafugaji Wilaya ya Kibaha mtaa wa Mwanalugali kimeweka mkakati wa kutumia ulinzi shirikishi ili kudhibiti vitendo hivyo.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na mwenyekiti wa chama hicho Haji Myaya alisema kuwa wamefikia maamuzi hayo baada ya kikao na wafugaji ambapo ndani ya wiki moja matukio matatu ya wizi yametokea

Myaya alisema kuwa changamoto ya wizi wa mifugo hasa ng'ombe umekuwa ukijitokeza mara kwa mara na kuwasababishia umaskini wafugaji na kuamua kuwa na walinzi hao.

"Tumekaa kikao na kukubaliana wanachama wote kutoa michango ya kila mwezi ili kuwalipa walinzi hao kupitia ulinzi shirikishi ili watulindie mifugo yetu na hata mali za wananchi,"alisema Myaya.

Alisema kuwa wezi hao huiba na kuwachinja ng'ombe na kisha kuchukua nyama na kwenda kuiuza sehemu zisizojulikana ambapo huacha vichwa na utumbo tu.

Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa nyama na mfugaji Aidan Mchiwa alisema kuwa kwa kushirikiana na chama cha wafugaji wamekuwa wakikabiliana na wezi wa mifugo kwa kuwa na mikakati mbalimbali ya kiulinzi.

Mchiwa alisema kuwa moja ya njia ni kuhakikisha nyama inayouzwa inakuwa imethibitishwa na mganga wa mifugo kwa kugongwa muhuri wa serikali ili kuepuka kuuza nyama ya wizi.

Alisema kuwa wafugaji wanashauriwa kuwa na mawasiliano ya simu ili linapotokea tukio la wizi wanaungana kwa pamoja na kufuatilia ng'ombe ambapo juzi walifanikiwa kurudisha ngombe watano ambao waliibiwa na kupelekwa Bagamoyo na wezi kukimbia.

"Tunashirikiana vizuri na jeshi la polisi katika kudhibiti wezi na kuwashauri wafugaji kutoa taarifa mapema wizi unapotokea ili kuwafuatilia wezi kabla hawajawachinja au kuwasafirisha mbali na kwenda kuwauza,"alisema Mchiwa.

Aidha aliwataka wafugaji kuwa na mahusiano mazuri na wafanyakazi wao wa mifugo kwa kuwalipa kwa wakati ili wasiingie vishawishi na kushirikiana na wezi kuiba mifugo.

No comments:

Post a Comment