Friday, September 8, 2023

WATAKA HATUA ZAIDI KUONGEZA MATUMIZI YA GESI

IMEELEZWA kuwa matumizi ya nishati ya gesi kwa ajili ya kupikia ni asilimia moja tu huku matumizi ya kuni na mkaa ikiwa ni asilimia 98.9 hapa nchini huku ikihitajika hatua za makusudi za kuzuia matumizi hayo ya miti ili kupunguza athari kubwa za kimazingira.

Aidha serikali imeombwa kuweka bei ya juu ya
upatikanaji wa vibali vya ukataji wa miti ili kupunguza matumizi ya mkaa na kuhamasisha matumizi ya gesi majumbani.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na ofisa Mahusiano wa kampuni ya Taifa Gesi Ambwene Mwakalinga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali waliotembelea eneo la ujazaji wa gesi ya (LPG) kwenye ghala lililopo Kigamboni.

Mwakalinga amesema kuwa matumizi ya kuni na mkaa ni makubwa sana hivyo kuna haja ya serikali kuweka jitihada za makusudi za kukabiliana na hali hiyo ili kusitokee mabadiliko ya Tabianchi ambayo yanasababisha athari ikiwemo ukosefu wa mvua na uharibifu wa mazingira.

Naye meneja wa ghala hilo la Kigamboni Juma Masese amesema kuwa Taifa Gesi ndiyo kampuni ya hifadhi kubwa ya gesi hapa nchini ambayo inamilikiwa na mzawa ambapo kwa sasa inahifadhi ujazo wa metriki tani 7,400 ambapo inatarajia kuwa kampuni ya kwanza Afrika kwa kuwa na hifadhi kubwa ya nishati hiyo ambayo huletwa na meli kutoka nchi zinazozalisha gesi duniani.

Kwa upande wake ofisa usalama wa kampuni hiyo Albert Bungayela amesema kuwa wanatoa elimu kwa mawakala ili nao watoe elimu kwa watumiaji kuwa makini katika matumizi ili kuepuka madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya gesi.


No comments:

Post a Comment