JESHI la Polisi Mkoani Pwani linamshikilia mkazi wa Kwa Mathias Wilayani Kibaha Janeth Dominick (26) kwa tuhuma za kumwagia chai ya moto sehemu mbalimbali za mwili dada wa kazi Filomena Erick (17).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Kibaha na Kamanda wa Polisi mkoani humo ACP Pius Lutumo ilisema kuwa mtuhumiwa alimuunguza dada huyo na chai aliyomwagia.
Lutumo amesema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 14 mwaka huu majira ya saa 2:00 asubuhi ambapo mtuhumiwa ni mwajiri wake alimuunguza maeneo ya shingoni, mkononi, kifuani na tumboni.
"Mtuhumiwa alifikia hatua hiyo kwa kumtuhumu kuiba unga, sukari na simu ya mkononi katika chumba cha mpangaji mwenzao,"amesema Lutumo.
Amesema kuwa mtuhumiwa atafikishwa kwenye mifumo ya kisheria mara upelelezi utakapokamilika kuhusiana na tukio hilo.
"Jeshi la polisi linatoa rai kwa watu wote wanaoishi na wadada wa kazi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani tukio hilo halikubaliki katika jamii na ni kinyume cha sheria,"amesema Lutumo
No comments:
Post a Comment