WAFANYABIASHARA wa soko la Uhindini Wilaya ya Chunya wameomba uboreshwaji wa huduma zikiwemo za miundombinu ya barabara maji na umeme ili waweze kutoa huduma kwa ubora kwa wateja wao.
Hayo yamebainishwa na wafanyabiashara wa wilaya hiyo wakati wa mkutano wa wafanyabiashara ulioongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Bw. Hamis Livembe September 7 wenye lengo la kupokea changamoto kero na maoni ya biashara ili kupatiwa ufumbuzi.
Mmoja wa wafanyabiashara wilayani hapo Qeen Mwasakela amesema kuwa changamoto ya umeme ina takribani miaka 10 tangu soko hilo kuanzishwa na kuiomba serikali kutatua kero hiyo.
Naye katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Tanga Ismail Masoud amewataka wafanyabiashara kueleza changamoto kwa mamlaka husika bila ya kuogopa ili zipatiwe ufumbuzi.
Katika hatua nyingine Masoud amewataka wafanyabiashara hao kutoungana na baadhi ya maofisa wa mamlaka mbalimbali ambao wanahujumu mipango ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hasan ya ukusanyaji wa mapato.
Amesema kuwa wasikubali kudanganywa kuwa watapunguziwa au kufutiwa kodi kwa kutakiwa kutoa rushwa ambapo mamlaka zinazohusika zikifuatilia hujikuta akiwa na deni kubwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Bw. Hamis Livembe amesema kuwa ukosefu wa huduma bora za msingi za kibiashara zinasababisha kushuka kwa biashara na ulipaji kodi kutofanyika vizuri na atahakikisha changamoto hizo zinafikishwa kwenye mamlaka husika ili kupatiwa ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment