WALIMU wanaofundisha somo la Hisabati Mkoani Pwani wametakiwa kutumia ufanisi umahiri na dhana stahiki kupitia mbinu za ufundishaji wa somo hilo ili kuongeza ufaulu.
Hayo yamesemwa Wilayani Kisarawe na Katibu Tawala (RAS) Mkoa wa Pwani Ramadhan Mchatta ambaye aliwakilishwa na Ofisa Elimu Mkoa Sara Mlaki wakati wa Mafunzo kwa viongozi wa elimu kuhusu uboreshaji ufundishaji na ujifunzaji wa umahiri wenye changamoto katika somo la hisabati kwa mkoa huo.
Mchatta amesema kuwa kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wanafunzi kwenye somo la hisabati ambapo utafiti umebaini baadhi ya wanafunzi kufanya vibaya kwenye mitihani ikiwemo ile ya Mock Wilaya na Mkoa.
Naye mtaalamu kiongozi wa Shule Bora Vicent Katabalo ameupongeza Mkoa wa Pwani kwa kutekeleza vizuri afua mbalimbali za mradi wa Shule Bora na kutaka waendeleze jitihada ili kufikia malengo yaliyowekwa ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi.
Kwa upande wake ofisa elimu mkoa wa Pwani Sara Mlaki amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha umahiri wa wa walimu na viongozi wa Elimu katika kutumia mbinu shirikishi za ufundishaji na ujifunzaji wa somo la Hisabati ili kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi wote.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Taasisi ya Elimu Tanzania kupitia Program ya Shule Bora ambayo inatekelezwa katika mikoa tisa ya Tanzania Bara kwa Ufadhili wa Serikali ya Uingereza na kwa Usimamizi wa Cambridge Education.
Mafunzo hayo yameendeshwa na wawezeshaji kutoka vyuo vya Ualimu vya Tukuyu na Mpwapwa ambapo washiriki wa mafunzo hayo ni viongozi wa Elimu kutoka katika ngazi ya Mkoa wakiwemo Walimu, Walimu wakuu, Maofisa Elimu Kata, Maofisa Elimu Awali na Msingi kutoka katika Halmashauri tisa na shule teule za Wilaya ya Kisarawe.
No comments:
Post a Comment