WANAFUNZI 42,000 kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha watafikiwa na mpango wa Shule Salama wenye lengo la kuhakikisha wanakuwa salama kuanzia shuleni na wawapo nyumbani.
Hayo yalisemwa na Ofisa Elimu Watu Wazima anayesimamia afya Shuleni Halmashauri ya Mji Kibaha Juliana Mwakatenya wakati wa mafunzo kwa wadau wa Shule Salama kwenye Halmashauri hiyo.
Mwakatenya alisema kuwa mpango huo uyazifikia shule zote za msingi za serikali na za binafsi na umelenga kuhakikisha usalama wa mwanafunzi kuanzia shuleni na nyumbani ili kumlinda na changamoto mbalimbali ikiwemo vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa.
Kwa upande wake mratibu wa Shule Salama Halmashauri ya Mji Kibaha Japhary Kambi alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia wadau kuwalinda watoto ili wafikie malengo yao ambapo wadau wakijua vikwazo vinavyowakabili wanafunzi itakuwa ni rahisi kukabiliana navyo na kutoa taarifa sehemu husika ili wanaofanya vitendo hivyo wachukuliwe hatua za kisheria.
Naye Chiku Abdul ofisa mwezeshaji wa mpango huo alisema kuwa matukio mengi ya vitendo vya ukatili yamekuwa hayaripotiwi na kufanya matukio kuongezeka kwani baadhi ya wazazi au walezi wa watoto wamekuwa wakimalizana pasipo kuyafikisha matukio hayo kwenye vyombo vya sheria.
Hatibu Omary mwenyekiti wa wasilishaji wa mada alisema kuwa wanaishukuru serikali kwa kuwapatia mafunzo ambapo waliyafanyia mkoani Morogoro na wao ndiyo wanawafundisha wadau wengine kuwa ulinzi na usalama wa mtoto ni jukumu la watu wote ndani ya jamii na kuwataka kutofumbia macho vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa watoto.
No comments:
Post a Comment