Tuesday, March 26, 2024
SERIKALI KUFUATILIA SUALA LA ELIMU NCHINI
Monday, March 25, 2024
VIONGOZI WAPYA WA KANISA WAPEWA NENO
Na Wellu Mtaki, Dodoma
Viongozi wa kanisa la Dayosisi Central Tanganyika (DCT ) Mtakatifu Paulo Parishi ya Ndachi Dodoma wamewataka viongozi waliosimwikwa katika Kanisa hilo kuwa mfano ili kujenga jamii yenye maadili.
Hayo yamebainishwa na Mchungaji wa Parishi ya Ndachi Msalato Dodoma Christopher Njiliho Leo Machi 24 ,2024 baada ya kumalizika kwa ibada ya kusimikwa kwa viongozi wa idara mbalimbali ndani ya kanisa hilo ambapo wamesema kuwa kanisa lina nafasi nzuri ya kujenga jamii bora.
"Ninawaomba sana viongozi muwe wa kwanza kuacha dhambi, kuacha vitendo vibaya ili muende kufundisha wengine ukiwa mfano watu watakusikiliza sana na watapokea ujumbe ambao utawapelekea ili kuzuia vitendo viovu,"amesema Njiliho.
Aidha amesema kuwa kanisa linatakiwa kuwa mfano wa kuigwa ili kuhakikisha linajenga Vijana walio imara kwa kuzingatia maadili na taratibu za Taifa la Tanzania.
Kwa upande wake Mlezi wa idara ya kina Mama Violeth Njiliho amesema kuwa Vijana wengi wamepotea kwa kukosa Maadili hivyo kama kanisa wanapenda kuhamasisha Vijana kushiriki semina mbalimbali ili kubadilisha mwenendo na kuongeza nguvu kazi kwa Taifa na kanisa .
"Vijana ni nguvu kazi ya Taifa pia ni nguvu kazi ya kanisa Vijana wengi wamepotea kwa kukosa maadili kama kanisa tunaenda kuhamasisha Vijana wetu waweze kupata semina mbalimbali ili waondoke katika hatua waliyonayo ya utandawazi ili warudi kumtegemea Mungu,"amesema Violeth
Naye Mhasibu wa parishi ya Ndachi Amos Mchoro amesema kuwa kanisa linategemea kuanzisha mradi wa Ujenzi wa frem za maduka ambayo yatasaidia kuinua pato la kanisa na muumini mmoja mmoja kwa kutoa na fursa zitokanazo na mradi huo.
"Mpango tulionayo kwa ajili ya Vijana wa mitaani tunategemea kuanzisha mradi wa kufungua frem za biashara kwa ajili ya kukodisha waumini wote na ambao sio waumini,"amesema Mchoro
Pia amesema kuwa kanisa lipo kwenye mchakato wa kutafuta namna ya kukopeshwa mikopo kwa vijana ili kuhakikisha kila kijana ananufaika na mkopo huo ili kuweza kujikwamua kiuchumi.
"Tunakusanya Vijana ambao wapo mtaani ili kuwavuta walijue neno la Mungu pamoja na kutafuta fedha na kuanza kujikopesha kwa watu ambao wanasali katika kanisa hili na wasio wa kanisa hili,"amesema Mchoro.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Vijana Parishi ya Ndachi Msalato Timotheo Hoya amewataka Vijana wamtumikie Mungu na waachane na vitendo rushwa, wizi, ulawiti pamoja na matumizi ya madawa ya kulevya.
"Vijana wa kanisa wamtumikie Mungu kwa kipindi hichi madam Tanzania kwa sasa inakumbana na matatizo mbalimbali kama matatizo ya rushwa, ukatili , wizi,na matumizi ya madawa ya kulevya,"amesema Hoya.
Awali Mwenyekiti wa Idara ya watoto Joyce Jackson amewahimiza wazazi kuhakikisha wanawakuwakumbusha watoto kwenda kanisani ili kuweza kulishika neno na kulitambua ili kuondokana na vitendo viovu vya ulawiti kwa watoto.
"Mtoto akitembea na neno kwa njia ya haki huwezi kumfanyia ulawiti kutokana na mtoto kutambua vitu viovu na anaishi ndani ya maadili pia nawasihi wazazi wawalete watoto wao makanisani nashangaa kuona mzazi anamwacha mtoto chini ya miaka 15 nyumbani bila kumhimiza kufika kanisani," amesema Jackson.
Kanisa la Dayosisi Central Tanganyika (DCT) la Mtakatifu Paulo Parishi ya Ndachi Dodoma limesimika viongozi 70 katika idara mbalimbali huku likiwa linahudumia wazee vijana na watoto.
Friday, March 22, 2024
WALIOKIUKA SHERIA YA MADINI MAOMBI YAO KUFUTWA
WAZIRI wa Madini Antony Mavunde amesema wamiliki waliokiuka na kutotekeleza Sheria ya Madini maombi na leseni zao zitafutwa ili kupisha waombaji wengine kupata fursa ya kuomba maeneo hayo.
Ametoa taarifa hiyo Leo Tarehe 22 March 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wamiliki waliomiliki Maeneo ya uchimbaji wa Madini bila kuyafanyia kazi.
Aidha amesema kuwa kwa wamiliki wa akaunti za uombaji na usimamizi wa leseni kwa njia ya mtandao ambao wameonesha matumizi mabaya ya mfumo huo kwa kuwasilisha maombi kwa lengo la kuhodhi maeneo bila kuendelea na kuratibu upatikanaji wa leseni akaunti zao zitasitishwa.
Amesema miongoni mwa makosa ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara ni pamoja na wamiliki wengi wa leseni kutoanza au kutoendeleza maeneo ya leseni zao na badala yake wanahodhi maeneo, hawalipi ada stahiki za leseni, hawawasilishi nyaraka muhimu kama Mpango wa Ushirikishwaji wa Watanzania
"Kutokana na kosa la kutolipa ada stahiki za leseni, kiasi cha takribani Shilingi bilioni 36 zinadaiwa kutoka kwa wamiliki na waliokuwa wamiliki wa Leseni za Utafutaji wa Madini, Leseni za Uchimbaji Mdogo wa Madini na Leseni za Uchimbaji wa Kati wa Madini,"amesema Mavunde.
Pia amesema kuwa Tume ya Madini imetoa Hati za Makosa kwa jumla ya leseni 59 kwa sababu wamiliki wake hawajatekeleza masharti na matakwa mbalimbali ya umiliki wa leseni husika Hivyo, taratibu za kufuta leseni hizo zinaandaliwa ili kuruhusu waombaji wengine kupata fursa ya kufanya uwekezaji.
"Vilevile katika uchambuzi uliofanya na Tume ya Madini imebainika kuwa, hadi Februari, 2024 kuna uwepo wa maombi 409 ambayo wamiliki wake wamelipa ada za maombi lakini hawajawasilisha nyaraka muhimu zinazoambatana na maombi hayo." Amesema Mavunde.
Katika atua ingine amesema kuwa uchambuzi uliofanywa na Tume ya Madini imebainika kuwa hadi Februari, 2024 kuna jumla ya maombi 2,180 ambayo hayajalipiwa ada stahiki za maombi pamoja na kubaini kuwa kuna watumiaji watano (5) wa mfumo wa uwasilishaji wa maombi kwa njia ya mtandao ambao wamekuwa wakitumia mfumo vibaya kwa kuwasilisha maombi bila kulipa ada stahiki.
Pia ametoa rai kwa wawekezaji wote wenye leseni za uwekezaji katika Sekta ya Madini kuzingatia matakwa ya Sheria ya Madini, Sura ya 123.
Aidha, Wizara ya Madini itaendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kufanya uwekezaji wenye tija na kukuza uchumi wa taifa letu kutokana na uvunaji wa rasilimali madini.
SERIKALI KUHAKIKISHA UJENZI KIWANDA USAFISHAJI MADINI LINATIMIA
Na Wellu Mtaki Dodoma
Waziri wa Madini Anthony Mavunde amewataka wachimbaji wa madini hasa yaliyokuwa na changamoto ya uchenjuaji na kulazimika kusafirishwa kwa mfumo wa makinikia, kuendelea kushirikiana kikamilifu na Serikali ili kuhakikisha lengo la ujenzi wa kiwanda cha usafishaji madini linatimia na linabaki kuwa alama ya ushindi katika usimamizi wa sekta ya madini.
Waziri Mavunde ameyasema hayo Machi 21,2024 Jijini Dodoma kwenye hafla ya kukabidhi leseni kubwa ya uchimbaji madini na leseni ya usafishaji madini ambapo ameongeza kuwa zoezi hilo linaenda kuongeza idadi ya leseni na kufikia 20.
“Ujenzi wa kiwanda cha multi metal refinery naamini itakuwa ni utatuzi wa changamoto iliyokuwepo kwa wachimbaji wa madini nchini kulazimika kusafirisha makinikia ya metali kwenda kwenye viwanda vya nje ya nchi kwa ajili ya uchakataji ili kupata zao la mwisho au kuuza madini katika hali ya makinikia kwa bei ya chini,”amesema Mavunde.
Aidha Waziri Mavunde ameongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa changamoto zinazojitokeza kwenye sekta ya madini nchini Wizara inaendelea kufanya mazungumzo na wawekezaji wa nyanja mbalimbali ikiwemo utafutaji, uchimbaji na ujenzi wa viwanda vya usafishaji madini ili kuingia ubia na watanzania jambo litakaloongeza wigo wa upatikanaji wa mitaji, utaalam pamoja na uhaulishaji wa teknolojia.
“Nitumie nafasi hii pia kutoa wito kwa wachimbaji na wamiliki wa migodi inayozalisha makinikia nchini kutumia kiwanda hiki pindi kitakapo kamilika ili kukuza fursa za ajira na mapato yatokanayo na rasilimali madini, ameongeza Mavunde.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha amemuahidi Waziri wa Madini Anthony Mavunde kuwa atatoa ushirikiano kwa mamlaka zote katika kuhakikisha Fungani ya Buzwagi inakuwa na mafanikio makubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Kahama.
RC Macha ameongeza kuwa wataendelea kuwahimiza wananchi wa Mkoa huo wa Shinyanga kuendelea kuchangamkia fursa zitakazojitokeza kupiti uwekezaji huo.
“Sambamba na uwekezaji mkubwa unaoenda kufanywa kule, na kama ambavyo tayari mmekwisha kunidokeza kuwa kampuni nyingi na kubwa zimekwisha onesha nia ya kuwekeza Mkoani Shinyanga sisi tunawihimiza wananchi wa pale wachangamkie fursa hii,”amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian amesema kupitia uwekezaji huo uliofanywa na Serikali utaenda kuleta fursa mbalimbali kwa wananchi wa mkoa huo ikiwemo kujipatia ajira.
Thursday, March 21, 2024
WAANDISHI WAASWA KUHAMASISHA WANAWAKE KUSHIKA NAFASI ZA UONGOZI
WAANDISHI wa Habari nchini wametakiwa kutumia kalamu zao kuhamasisha wanawake kushika nafasi mbalimbali za uongozi na kwenye ngazi za maamuzi kwani uwekezaji kwa wanawake ni fursa na msingi wa kujenga jamii jumuishi.
CCM PWANI YAIBUKA NA USHINDI UDIWANI
Wednesday, March 20, 2024
MAMLAKA ZA MAJI ZATAKIWA KULIPA MADENI YATOKANAYO NA TOZO
SERIKALI kupitia wizara ya Maji imezitaka Mamlaka za Maji zote zinazodaiwa kuwasilisha deni la tozo zake ili kuiwezesha EWURA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi hii nikutokana na deni la tozo kwa Mamlaka za Maji kufikia takribani shilingi bilioni 4.6.
Akizindua Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa kipindi cha mwaka 2022/23 ambayo ni ya 15 kutolewa na EWURA, Mhandisi Mwajuma Waziri Katibu Mkuu wa wizara ya Maji amezitaka mamlaka hizo zinazodaiwa ankara za maji zilipe madeni yake mapema ili kuziwezesha kujiendesha na kuweza kutoa huduma kwa ufanisi.
"Kwa Mamlaka za Maji ambazo utendaji wake hauridhishi niseme wazi hatutasita kuzichukulia hatua, nafahamu kuwa baadhi zinashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za bei ya maji kuwa chini ikilinganishwa na gharama za uendeshaji". Amesema.
Aidha,Katibu mkuu huyo amewasisitiza watendaji wanaohusika katika usimamizi wa miradi ya Maji nchini kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa Sheria.
"Kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi hii, wahakikishe wanaikamilisha kwa wakati'tunafahamu moja ya changamoto zinazoikabili sekta ya maji nchini ni pamoja na kuchelewa kutekelezwa kwa miradi,sitovumilia kuona hili likijitokeza katika miradi hii mikubwa na yenye maslahi makubwa kwa taifa"Amesisitiza
Licha ya hayo,ameziagiza Mamlaka za Maji kushirikiana na Halmashauri zote za Wilaya kuhamasisha uvunaji wa maji ya mvua katika ngazi zote hasa katika kipindi hiki ambapo mvua zinaendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.
"Tumejionea mvua hizi katika baadhi yua maeneo zimeleta madhara makubwa, hivyo basi,endapo tutavuna maji haya tutapunguza kama siyo kuondoa kabisa athari zake na pia kutaiwezesha nchi yetu na wananchi kuwa na akiba ya maji ambayo yatatusaidia kipindi cha ukame". Amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt. James Andilile amesema taarifa iliyozinduliwa leo ni ya 15 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo miaka 18 iliyopita na inahusisha uchambuzi wa utendaji wa mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira 85 zikiwemo; mamlaka 25 za mikoa, saba (7) za miradi ya kitaifa, 47 za wilaya na Sita (6) za miji midogo.
Dkt.Andilile amesema Utendaji wa mamlaka za maji na usafi wa mazingira umeendelea kuimarika ambapo kwa mwaka 2022/23, Mamlaka za Maji 78 kati ya 85 zilipata alama kuanzia wastani hadi vizuri sana katika utendaji wa ujumla ikilinganishwa na mamlaka 77 kati ya 90 kwa mwaka 2021/22.
Ameyataja Maeneo yaliyoimarika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mwaka 2021/22 kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha maji yaliyozalishwa kutoka mita za ujazo milioni 393 hadi 400 sawa na asilimia 1.8 , kuimarika kwa uwiano kati ya watumishi na wateja kutoka 4.2 hadi 3.8 kwa kila wateja 1000 , kuimarika kwa Uwiano wa maunganisho yaliyofungwa dira za maji kufikia asilimia 92 ikilinganishwa na asilimia 90 ,kuongezeka kwa kiwango cha ubora wa maji yanayosambazwa kwa wateja kutoka asilimia 91 hadi 94;
Maeneo mengine ni kuongezeka kwa wateja wa maji wa majisafi kutoka kutoka 1,385,485 hadi 1,532,362 sawa na asilimia 11 na kuongezeka kwa wateja wa mtandao wa uondoaji majitaka kutoka wateja 55,996 hadi wateja 56,899 sawa na asilimia 16.
“Nafahamu kuwa mafanikio hayo hayakuja bure. Naomba nitumie fursa hii kumpongeza na kumshukuru Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wewe Mheshimiwa Waziri kwa usimamizi wako mahiri wa sekta ya maji kwa kufanya uwekezaji mkubwa kwa lengo la kumtua mama ndoo kichwani na kuimarisha ustawi wa watanzania wote, kwani maji ni uhai,” amesema Dkt. Andilile
Uzinduzi huo umekwenda sambamba na utoaji wa tuzo mbalimbali Kwa Mamlaka zilizofanya vizuri huku zikigawanywa katika makundi Matatu tofauti kulingana na idadi ya wateja inayowahudumia ambapo kundi la kwanza ni Mamlaka za maji zenye wateja chini ya 5000, kundi la pili ni mamlaka za maji zenye wateja chini kati ya 5000 na 20,000 na kundi la Tatu ni mamlaka za maji zenye wateja zaidi ya 20,000.






