Na Wellu Mtaki, Dodoma
Viongozi wa kanisa la Dayosisi Central Tanganyika (DCT ) Mtakatifu Paulo Parishi ya Ndachi Dodoma wamewataka viongozi waliosimwikwa katika Kanisa hilo kuwa mfano ili kujenga jamii yenye maadili.
Hayo yamebainishwa na Mchungaji wa Parishi ya Ndachi Msalato Dodoma Christopher Njiliho Leo Machi 24 ,2024 baada ya kumalizika kwa ibada ya kusimikwa kwa viongozi wa idara mbalimbali ndani ya kanisa hilo ambapo wamesema kuwa kanisa lina nafasi nzuri ya kujenga jamii bora.
"Ninawaomba sana viongozi muwe wa kwanza kuacha dhambi, kuacha vitendo vibaya ili muende kufundisha wengine ukiwa mfano watu watakusikiliza sana na watapokea ujumbe ambao utawapelekea ili kuzuia vitendo viovu,"amesema Njiliho.
Aidha amesema kuwa kanisa linatakiwa kuwa mfano wa kuigwa ili kuhakikisha linajenga Vijana walio imara kwa kuzingatia maadili na taratibu za Taifa la Tanzania.
Kwa upande wake Mlezi wa idara ya kina Mama Violeth Njiliho amesema kuwa Vijana wengi wamepotea kwa kukosa Maadili hivyo kama kanisa wanapenda kuhamasisha Vijana kushiriki semina mbalimbali ili kubadilisha mwenendo na kuongeza nguvu kazi kwa Taifa na kanisa .
"Vijana ni nguvu kazi ya Taifa pia ni nguvu kazi ya kanisa Vijana wengi wamepotea kwa kukosa maadili kama kanisa tunaenda kuhamasisha Vijana wetu waweze kupata semina mbalimbali ili waondoke katika hatua waliyonayo ya utandawazi ili warudi kumtegemea Mungu,"amesema Violeth
Naye Mhasibu wa parishi ya Ndachi Amos Mchoro amesema kuwa kanisa linategemea kuanzisha mradi wa Ujenzi wa frem za maduka ambayo yatasaidia kuinua pato la kanisa na muumini mmoja mmoja kwa kutoa na fursa zitokanazo na mradi huo.
"Mpango tulionayo kwa ajili ya Vijana wa mitaani tunategemea kuanzisha mradi wa kufungua frem za biashara kwa ajili ya kukodisha waumini wote na ambao sio waumini,"amesema Mchoro
Pia amesema kuwa kanisa lipo kwenye mchakato wa kutafuta namna ya kukopeshwa mikopo kwa vijana ili kuhakikisha kila kijana ananufaika na mkopo huo ili kuweza kujikwamua kiuchumi.
"Tunakusanya Vijana ambao wapo mtaani ili kuwavuta walijue neno la Mungu pamoja na kutafuta fedha na kuanza kujikopesha kwa watu ambao wanasali katika kanisa hili na wasio wa kanisa hili,"amesema Mchoro.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Vijana Parishi ya Ndachi Msalato Timotheo Hoya amewataka Vijana wamtumikie Mungu na waachane na vitendo rushwa, wizi, ulawiti pamoja na matumizi ya madawa ya kulevya.
"Vijana wa kanisa wamtumikie Mungu kwa kipindi hichi madam Tanzania kwa sasa inakumbana na matatizo mbalimbali kama matatizo ya rushwa, ukatili , wizi,na matumizi ya madawa ya kulevya,"amesema Hoya.
Awali Mwenyekiti wa Idara ya watoto Joyce Jackson amewahimiza wazazi kuhakikisha wanawakuwakumbusha watoto kwenda kanisani ili kuweza kulishika neno na kulitambua ili kuondokana na vitendo viovu vya ulawiti kwa watoto.
"Mtoto akitembea na neno kwa njia ya haki huwezi kumfanyia ulawiti kutokana na mtoto kutambua vitu viovu na anaishi ndani ya maadili pia nawasihi wazazi wawalete watoto wao makanisani nashangaa kuona mzazi anamwacha mtoto chini ya miaka 15 nyumbani bila kumhimiza kufika kanisani," amesema Jackson.
Kanisa la Dayosisi Central Tanganyika (DCT) la Mtakatifu Paulo Parishi ya Ndachi Dodoma limesimika viongozi 70 katika idara mbalimbali huku likiwa linahudumia wazee vijana na watoto.
No comments:
Post a Comment