Thursday, March 14, 2024

KATA YA TANGINI YAPATA MILIONI 120 KWA AJILI YA ZAHANATI

KATA ya Tangini Wilayani Kibaha imepata kiasi cha shilingi milioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ambapo itakapokamilika itahudumia watu 20,146.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Kibaha Diwani wa Kata ya Tangini Mfalme Kabuga amesema kuwa tayari fedha hizo zimetokana na mapato ya ndani.

Kabuga amesema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo unatarajia kuanza wakati wowote kuanzia sasa na tayari eneo limepatikana eneo la mtaa wa Kilimahewa.

"Wananchi wa Kata hiyo wanapata huduma za kiafya kwenye Hospitali za Tumbi, Mkoani na Pangani ambapo hutumia gharama kubwa zinazofikia kiasi cha shilingi 4,000 hadi 6,000 za pikipiki kufika kwenye huduma za afya,"amesema Kabuga.

Amesema kuwa Zahanati hiyo itajengwa na serikali hadi kukamilika na itakapokamilika itawapunguzia gharama za usafiri na pia kuepuka kwenda moja kwa moja kwenye Hospitali kubwa ambapo gharama zinakuwa ni kubwa endapo hawajaanzia ngazi ya chini.

"Tunaishukuru serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan na Mbunge wetu Silvestry Koka na Madiwani wa Halmashauri ya Mji Kibaha ambao wametufanyia mambo makubwa katika kukabili changamoto za wananchi,"amesema Kabuga.

Ametaja mitaa itakayonufaika na zahanati hiyo kuwa ni Maili Moja B, Tangini, Kilimahewa, Machinjioni na Mtakuja na mtaa jirani wa Muheza toka Kata ya Maiili Moja.

No comments:

Post a Comment