Monday, March 11, 2024

KATA YA MAILI MOJA WAELEZEA MAFANIKIO NA CHANGAMOTO

KATA ya Maili Moja Wilayani Kibaha Mkoani Pwani imeelezea mafanikio na changamoto huku wakiitaka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kukarabati miundombinu ya barabara ambayo imeharibika vibaya.

Diwani wa Kata hiyo Ramadhan Lutambi ameelezea baadhi ya mafanikio na changamoto mbele ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha Moses Magogwa ambaye alimwakilisha mkuu wa Wilaya ya Kibaha wakati wa mkutano wa hadhara kwenye mtaa wa Uyaoni.

Lutambi amesema baadhi ya mafanikio ni kwenye sekta ya elimu ambapo kwenye sekondari ya Bundikani kwenye matokeo ya kidato cha nne mwaka jana wamefanikiwa kuondoa daraja sifuri na ujenzi wa madarasa mapya.

Amesema kwa upande wa shule za msingi wamefanikiwa kuanzisha shule mpya ya Muheza, shule za Maendeleo na Maili Moja zimejengewa madarasa mapya, kwa upande wa serikali za mitaa kujenga ofisi zake badala ya kupanga.

"Kuna baadhi ya changamoto lakini kubwa ni miundombinu ya barabara hii ni tatizo kwa mitaa yote suala la urasimishaji, umeme kukatika mara kwa mara, baadhi ya maeneo kukosa maji na umeme na mikopo ya kausha damu,"amesema Lutambi.

Kwa upande wake katibu tawala wa Wilaya ya Kibaha Moses Magogwa amesema kuhusu changamoto ya barabara atawaelekeza Tarura ili wakae na wananchi ili kuangalia vipaumbele vya barabara ili zianze kufanyiwa marekebisho.

Magogwa amesema kuhusu urasimishaji wote waliopewa hiyo kazi wakutane naye ofisini ili kuangalia namna ya kutatua changamoto hiyo ili kuondoa malalamiko ya wananchi.

Amesema kuhusu mikopo ya kausha damu viongozi wa mitaa wakae na wamiliki wa taasisi hizo za mikopo ili kuangalia namna ya kudai marejesho badala ya kuwadhalilisha watu.

Ameongeza kuwa serikali inasikiliza kero za wananchi ili kuzitatua kwani Rais Dk Samia Suluhu Hassan anapambana kuhakikisha wananchi wanaishi kwenye mazingira mazuri.

No comments:

Post a Comment