Friday, March 22, 2024

WALIOKIUKA SHERIA YA MADINI MAOMBI YAO KUFUTWA

 

WAZIRI wa Madini Antony Mavunde amesema wamiliki waliokiuka na kutotekeleza Sheria ya Madini maombi na leseni zao zitafutwa ili kupisha waombaji wengine kupata fursa ya kuomba maeneo hayo.

Ametoa taarifa hiyo Leo Tarehe 22 March 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wamiliki waliomiliki Maeneo ya uchimbaji wa Madini bila kuyafanyia kazi. 

Aidha amesema kuwa  kwa wamiliki wa akaunti za uombaji na usimamizi wa leseni kwa njia ya mtandao ambao wameonesha matumizi mabaya ya mfumo huo kwa kuwasilisha maombi kwa lengo la kuhodhi maeneo bila kuendelea na kuratibu upatikanaji wa leseni akaunti zao zitasitishwa. 

Amesema miongoni mwa makosa ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara ni pamoja na wamiliki wengi wa leseni kutoanza au kutoendeleza maeneo ya leseni zao na badala yake wanahodhi maeneo, hawalipi ada stahiki za leseni, hawawasilishi nyaraka muhimu kama Mpango wa Ushirikishwaji wa Watanzania

"Kutokana na kosa la kutolipa ada stahiki za leseni, kiasi cha takribani Shilingi bilioni 36 zinadaiwa kutoka kwa wamiliki na waliokuwa wamiliki wa Leseni za Utafutaji wa Madini, Leseni za Uchimbaji Mdogo wa Madini na Leseni za Uchimbaji wa Kati wa Madini,"amesema Mavunde.

Pia amesema kuwa Tume ya Madini imetoa Hati za Makosa kwa jumla ya leseni 59 kwa sababu wamiliki wake hawajatekeleza masharti na matakwa mbalimbali ya umiliki wa leseni husika Hivyo, taratibu za kufuta leseni hizo zinaandaliwa ili kuruhusu waombaji wengine kupata fursa ya kufanya uwekezaji.

"Vilevile katika uchambuzi uliofanya na Tume ya Madini imebainika kuwa, hadi Februari, 2024 kuna uwepo wa maombi 409 ambayo wamiliki wake wamelipa ada za maombi lakini hawajawasilisha nyaraka muhimu zinazoambatana na maombi hayo." Amesema Mavunde.

Katika atua ingine amesema kuwa uchambuzi uliofanywa na Tume ya Madini imebainika kuwa  hadi Februari, 2024 kuna jumla ya maombi 2,180 ambayo hayajalipiwa ada stahiki za maombi pamoja na kubaini kuwa kuna watumiaji watano (5) wa mfumo wa uwasilishaji wa maombi kwa njia ya mtandao ambao wamekuwa wakitumia mfumo vibaya kwa kuwasilisha maombi bila kulipa ada stahiki. 

Pia ametoa rai kwa wawekezaji wote wenye leseni za uwekezaji katika Sekta ya Madini kuzingatia matakwa ya Sheria ya Madini, Sura ya 123. 

Aidha, Wizara ya Madini itaendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kufanya uwekezaji wenye tija na kukuza uchumi wa taifa letu kutokana na uvunaji wa rasilimali madini.

No comments:

Post a Comment