Tuesday, March 12, 2024

EWURA KUMTUA MWANAMKE KUNI KICHWANI

Na Wellu Mtaki, Dodoma

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dkt. James Andilile,amesema mamlaka hiyo ina wajibu kuhakikisha wanamtua mwanamke kuni na mkaa kichwani kwa kuhakikisha wanatoa leseni kwa wakati kwa wawekezaji wanaokuja nchini kuwekeza katika nishati safi ya kupikia.

Dkt. Andilile ameyasema hayo Machi 9,2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la Mamlaka hiyo kwenye Kongamano la wanawake la kugawa mitaji na vitendea kazi vya nishati safi ya kupikia.

Amesema taifa bado linatumia nishati isiyosafi kwa kupikia hivyo EWURA itahakikisha ina wajibu wa kuhakikisha inatekeleza mikataba ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza ikiwemo uharibifu wa mazingira na madhara ya afya yanayosababidhwa na moshi wakati wa matumizi ya kuni na mkaa.

“EWURA tutahakikiha tunahamasisha uwekezaji katika nishati safi kwa kutoa leseni kwa wawekezaji kwa wakati ili wawekeze katika eneo hilo, pia tunaangalia upatikanaji wake katika maeneo mengi kwa kuangalia mwenendo wa bei za bidhaa hiyo,” amesema Dkt. Andilile.

Ameongeza kuwa:”Sisi kama EWURA tutahakikisha kama ilivyo dhamira ya Rais kumtua ndoo mama kichwani, tutamtua mwanamke kuni kichwani kwa kuhakikisha anatumia nishati ambayo itamrahisishia kupata maendeleo badala ya kuhangaika na nishati chafu ya kupikia,”.

No comments:

Post a Comment