Thursday, March 21, 2024

WAANDISHI WAASWA KUHAMASISHA WANAWAKE KUSHIKA NAFASI ZA UONGOZI

WAANDISHI wa Habari nchini wametakiwa  kutumia kalamu zao kuhamasisha wanawake kushika nafasi mbalimbali za  uongozi na kwenye ngazi za maamuzi kwani uwekezaji kwa wanawake ni fursa na msingi wa kujenga jamii jumuishi. 

Hayo yamesemwa leo Machi Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Lilian Liundi wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya uandishi unaozingatia jinsia hasa juu ya kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika uongozi.

Liundi amesema kuwa Tanzania imeweka historia ya kuwa na Rais mwanamke kwa mara ya kwanza Dk Samia Suluhu Hassan ambaye ameonyesha dhamira ya kuongeza usawa wa kijinsia.

"Pia tumesha kuwa na Maspika wa Bunge wawili wanawake ambao ni Anne Makinda na Dk Tulia Ackson na mawaziri wanawake walioshika nafasi katika wizara zinazoaminika kuwa ni za wanaume kama Wizara ya Ulinzi-Stigomena Tax, Wizara ya Mambo ya nje, Liberata Mulamula pia katibu wa Bunge Nenelwa Mhambi pia historia ya kuwa na mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Zuhura Yunus,"amesema Liundi.

Kwa upande wake Ofisa Habari na Mawasiliano TGNP Monica John amesema kuwa wamekuwa wakishirikiana na wadau mbalimbali katika uchechemuzi juu ya sera na bajeti zinazozingatia masuala ya jinsia na shughuli zao zinahusisha tafiti mbalimbali ili kuibadilisha jamii juu ya changamoto na mafanikio kwa kuwa na ushirikiano baina ya wanajamii na viongozi.

Mradi huo unatekelezwa kwenye Halmashauri za Dar es Salaam ni Jiji la Dar es Salaam, Temeke na Kinondoni, Pwani ni Kisarawe, Chalinze na Kibaha Mjini, Lindi ni Ruangwa, Nachingwea na  Mtwara ni Mikindani, Mtwara na Tandahimba na Mafunzo hayo ya siku tatu yanaratibiwa na TGNP kwa kushirikiana na TADIO kwa udhamini wa shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women). 


No comments:

Post a Comment