Thursday, March 21, 2024

CCM PWANI YAIBUKA NA USHINDI UDIWANI

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Pwani kimeshinda Kata zote tatu kwenye chaguzi ndogo zilizofanyika baada ya madiwani wa Kata hizo kufariki dunia.

Chaguzi hizo zilizofanyika kwenye kata tatu za Fukayosi Wilaya ya Bagamoyo Kibaha Mjini na Mlanzi Wilaya ya Kibiti ambapo kote imeshinda wapinzani kwa zaidi ya asilimia 90 ya kura zilizopigwa.

Kwenye uchaguzi wa Kata ya Fukayosi Wilaya ya Bagamoyo mgombea wa CCM Mrisho Some amepata kura 5,883 kati ya kura halali 5,960 sawa na asilimia 98.7 huku vyama vingine vikiwa ni CCK, DEMOKRASIA MAKINI, UDP na UMD.

Katika uchaguzi wa Kata ya Msangani Kibaha Mjini Yohana Gunze alishinda kwa kupata kura 5,862 kati ya kura halali 5,909 zilizopigwa sawa na asilimia 99.2 na kuvishinda vyama vya ADA - TADEA, CCK, DEMOKRASIA MAKINI, DP, N.R.A, UMD na UPDP.

Naye mgombea wa CCM Athumani Mketo Kata ya Mlanzi Wilaya ya Kibiti amepata kura 1,592 kati ya kura halali 1,732 sawa na asilimia 91.9 ambapo vyama vingine vikivyoshiriki ni ACT - WAZALENDO, CUF, DEMOKRASIA MAKINI, N.R.A, UDP, UMD na UPDP.

Akizungumzia ushindi huo Katibu wa Siasa Uenezi na Mafunzo CCM Mkoa wa Pwani David Mramba alisema kuwa ushindi wa CCM ni ishara njema kuelekea kwenye chaguzi zijazo kwani wananchi wana imani kubwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dk Samia Suluhu Hassan.

Mramba alisema kuwa kwenye uchaguzi ujao wa mwakani wa serikali za mitaa na vitongoji watahakikisha wanapata ushindi wa kishindo kwani huu mdogo ni kama mazoezi kwao.


No comments:

Post a Comment