Tuesday, March 12, 2024

WAFANYABIASHARA WA DODOMA WAIOMBA SERIKALI KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BIASHARA





Na Anna Misungwi, Dodoma 

WAFANYABIASHARA wa Mkoa wa Dodoma waiomba serikali kurekebisha miundombinu ya soko la Machinga Complex pamoja  soko la Mavunde  lililopo Kata ya Chang'ombe ambapo kipindi cha mvua maji huingia na biashara kuharibika.

Hayo yamesemwa na wafanyabiashara wa masoko hayo Tarehe 11 Machi 2024 wakati wa ziara ya mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Hamis Livembe, kwenye ziara iliyolenga kupokea changamoto, kero na maoni ya wafanyabiashara.

Mmoja wa wafanyabiashara Abdalla Ramadhan amesema kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na miundombinu ya soko kwani maji yanaingia na hivyo kusababisha bidhaa kuharibika.

Ramadhan amesema kuwa pia wanaomba kushushwa kwa ushuru kutoka 1,000 na kuwa 500 kwenye kizimba kwenye soko la Machinga Complex ambapo kizimba kimoja kinaweka wafanyabiashara wawili kwani ushuru wanaolipa unasababisha kushuka kwa biashara zao.

"Wafanyabiashara kipato chetu kinashuka tunaimomba serikali itusaidie kwani kizimba kimoja tunakaa watu wawili na kila mtu kwenye kizimba analipa shilling 1,000 ambapo watu wawili ni shilling 2,000 tunaomba tupunguziwe tulipe shilling 500 kwa kila mtu,"amesema Ramadhan.

Amesema wanaiomba serikali kuacha kuwafungia vizimba kutokana na hali ya wafanyabiashara kudaiwa kulipia ushuru kwani kizimba kikifungwa husababisha kukosa mapato kwa wafanyabiashara na serikali kwa ujumla.

"Tunafungiwa vizimba sababu ya mtu kama hajalipa ushuru siku moja au mbili kitendo ambacho wengi wanashidwa kuja kugomboa maana unapofungiwa lazima uje utoe fedha ndo ufunguliwe tunaomba serikali itusaidie,"wamesema wafanyabiashara hao.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Hamis Livembe amesema kuwa lengo la kuja ni kupokea changamoto, kero na maoni na changamoto ambazo zinaweza kutolewa majibu zinatolewa ufafanuzi na ambazo majibu hawana watazipeleka sehemu husika ili kuzitafutia ufumbuzi.

Livembe ametoa wito kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanakuwa wamoja katika kushughulikia matatizo kwa umoja.

No comments:

Post a Comment