Tuesday, March 26, 2024

SERIKALI KUFUATILIA SUALA LA ELIMU NCHINI

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Maofisa Elimu Kata nchini kufuatilia maendeleo ya shule kwa kuwatembelea walimu na kusikiliza kero zao

Aidha amewataka walimu kuhakikisha wanafanya tathmini ya uelewa wa wanafunzi kwa kuwapatia mazoezi mengi.

Majaliwa ameyasema hayo Machi 25, 2024   kwenye ukumbi wa TAG Mipango Jijini Dodoma wakati wa kilele cha Juma la wadau wa Elimu Mkoa.

Amesema maofisa elimu hao wafuatilie masuala ya walimu na kutatua changamoto zao ili wafanye kazi vizuri.

"Walimu nanyi hakikisheni mnafanya tathmini ya uelewa wa wanafunzi kwa kuwapatia mazoezi mengi kadri iiwezekanavyo,"amesema Majaliwa.

Fedha zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo ya Elimu, zitumike kwa ajili hiyo,"amesisitiza Majaliwa.

Amebainisha kuwa Kauli mbiu ya mkutano huo inakwenda sambamba na Sera ya Elimu ya nchi inayosisitiza Uwajibikaji, Utoaji wa Elimu Bora ni vipaumbele vya nchi. 

"Serikali yetu inaimarisha mazingira ya utoaji Elimu kwa kuboresha miundombinu na Elimu bila ada kwani mpaka Sasa shilingi Trilioni 1 zimetolewa kufanikisha hili,"amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu ameipongeza Dodoma kwa kuandaa Mkutano huo kwani unakwenda sambamba na Sera ya Elimu ya nchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema Serikali ya awamu ya Sita imefanya mambo mengi kwenye sekta ya Elimu.

Senyamule amesema kuwa wanamshukuru Rais kwa kuinua sekta ya Elimu Dodoma kwani wameimarika sana kipindi cha miaka hii mitatu Dodoma imepanda ufaulu wa darasa la saba na kuingia kumi bora kitaifa mwaka 2022 kwa ufaulu kupanda kutoka 83% mwaka 2022 hadi 87%mwaka 2023 na wameanza kuweka mikakati ya Mkoa kuhakikisha kila mwaka ufaulu unaongezeka.

Ametaja mafanikio yaliyopatikana kipindi hiki kuwa ni ujenzi wa miundombinu ya elimu iliyogharimu shilingi bilioni 92.4 , miradi ya BOOST shilingi bilioni 10.6 iliyowezesha ujenzi wa madarasa 196 na matundu ya vyoo 154 fedha nyingine ni kutoka miradi ya SEQUIP, SWASH, TEA , EP4R na mingine mingi ambayo kwa pamoja imeboresha kiwango cha elimu.

Mkutano wa wadau wa Elimu Mkoa wa Dodoma umefuatia matukio kadhaa yaliyofanyika kwa Juma zima ikiwemo kukimbia mchaka mchaka kwa wanafunzi, uzinduzi wa Bonanza la michezo, ugawaji wa mipira 1000 kwa shule za Msingi za Mkoa kutoka Shirikisho la michezo nchini (TFF).

Pia Juma hilo limewezesha uzinduzi wa kwaya ya Mkoa wa Dodoma, midahalo kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari na kufunga mafunzo kwa wahitimu wa skauti Mkoa.

Juma la wadau wa Elimu Mkoa wa Dodoma limefikia kilele chake likiongozwa na kauli mbiu ya "Uwajibikaji wangu ni msingi wa kuinua ubora wa Elimu na ufaulu Dodoma".

Lengo hasa la Mkutano huo ni kujadili namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Elimu Mkoa wa Dodoma pamoja na kuweka mikakati ya kuinua Taaluma na ufaulu kimkoa pamoja na kuzindua rasmi Mpango Mkakati wa Elimu Mkoa.

No comments:

Post a Comment