Monday, February 5, 2024

MWENDAPOLE B KUJENGA SHULE YA MSINGI


MTAA wa Mwendapole B Wilayani Kibaha uko kwenye hatua za mwisho katika kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi ili kuwapunguzia changamoto watoto wa mtaa huo kugongwa na magari wakivuka kwenda shule iliyoko mtaa jirani.

Aidha wanafunzi wanaotoka mtaa huo hutembea umbali wa kilometa mbili kwenda na kurudi hivyo kuwa na uhitaji wa shule ili kuwapunguzia umbali mrefu kwenda shule.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha Mwenyekiti wa Mtaa huo Abubakary Matumla amesema kuwa mtaa huo una shule za msingi na sekondari za watu binafsi ambazo ni wazazi wachache wenye uwezo wa kuwapeleka watoto wao kusoma hapo.

"Tayari eneo limepatikana lina ukubwa wa hekari nne ambalo ni la mtu binafsi ambaye inabidi alipwe ndipo aliachie hivyo kuna makubaliano na Halmashauri ya Mji wampatie eneo lingine ili apishe hapo tuko hatua za mwisho za mabadilishano,"amesema Matumla.

Matumla amesema kuwa tayari wana tofali zaidi ya 4,000 kwa ajili ya ujenzi huo hivyo wanasubiri tu Halmashauri wampatie eneo lingine ili waanze ujenzi wa shule hiyo ambayo itawaondolea changamoto ya kugongwa au kusoma mbali.

"Wananchi wameshachanga fedha kiasi cha shilingi milioni 1.6 ambapo tunashirikiana na diwani ili kufanikisha kupata eneo hilo na matumaini ni makubwa,"amesema Matumla.

LATRA YACHUKUA HATUA KWA DALADALA ZINAZOKIUKA TARATIBU ZA USAFIRISHAJI/KUKATISHA RUTI

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Pwani imeyachukulia hatua za kisheria mabasi madogo Daladala 53 kutokana na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukatisha safari.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na ofisa leseni na usajili wa Mamlaka hiyo Geofrey Mashishi alipozungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake.

Mashishi amesema kuwa hatua hizo zimechukuliwa kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita Desemba mwaka jana na Januari mwaka huu kwa Daladala zinazofanya safari ndani ya Mkoa huo.

"Hatua hizo tumezichukuwa kwa wasafirishaji hao kwa sababu ya kukiuka masharti ya leseni zao kwa makosa mbalimbali mengine yakiwa ni kutotoa tiketi, kuzidisha nauli na mengine ambayo ni kinyume na taratibu za usafirishaji,"amesema Mashishi.

Amesema kuwa ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wasafirishaji wanaokiuka masharti ya leseni zao kunahitajika ushirikiano baina yao na wadau wakiwemo abiria.

"Sekta ya usafirishaji ina changamoto nyingi na tumekuwa tukifanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa kwashirikiana na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha wasafirishaji wanafuata kanuni, sheria na taratibu za usafirishaji ili kuondoa malalamiko,"amesema Mashishi.

Aidha amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa abiria ili kujua haki zao na wasafirishaji kujua wajibu wao wanapotekeleza majukumu yao kupitia vyombo vya habari.

"Ukaguzi wa kufuatilia ni endelevu hivyo ni vema wasafirishaji wakazingatia masharti ya leseni zao ili kuondoa changamoto zisizo za lazima kwa wadau wa usafiri,"amesema Mashishi.




Sunday, February 4, 2024

LIKUNJA CUP ROBO FAINALI KUTIMUA VUMBI FEBRUARI 7


 MAashindano ya Likunja Cup hatua ya Robo Fainali yataanza kutimua vumbi Februari 7 uwanja wa Shule ya Msingi Zegereni kwa kuzikutanisha Misugusugu Fc na Veterani Fc kwa mujibu wa Rashid Likunja 

ATAKA MIKOPO ASILIMIA 10 YA HALMASHAURI IKOPESHE VIJANA WALIOACHA MATUMIZI DAWA ZA KULEVYA

HUKU Serikali ikiendelea na mchakato wa namna ya utoaji mikopo ya asilimia 10 za Halmashauri imeombwa kuangalia namna ya kuvikopesha vikundi vya waraibu wa dawa za kulevya ili wafanye shughuli za ujasiriamali.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Yohana Kilonzo Mkurugenzi wa Taasisi ya (OYARB) inayowahudumia watu waliokuwa wakitumia dawa za kulevya na kuacha na sasa wanatumia dawa za Methadoni zinazosaidia kuwarudisha katika hali yao ya kawaida ambapo kituo hicho kina vijana 500.

Kilonzo amesema kuwa watumiaji hao wanapokuwa hawana shughuli ya kufanya ni rahisi kurudia kutumia dawa za kulevya hivyo kuna haja ya kuwapatia shughuli za kufanya ili waweze kujipatia kipato.

"Wakati wakiendelea na tiba tunawafundisha shughuli za ujasiriamali ambapo wana mradi wa uuzaji wa sabuni za maji lengo wakitoka hatua hii wawe na uwezo wa kujitegemea ndiyo sababu tunaona nao wafikiriwe kwenye hiyo mikopo wapewe upendeleo,"amesema Kilonzo

Amesema kuwa kwa baadhi ya waliofuzu tiba hiyo baada ya kutumia Methadoni kwa kipindi cha miaka miwili ambazo wanapewa Hospitali ya Mkoa ya Rufaa ya Tumbi wamewachukua na kazi yao ni kufundisha juu ya athari na kuachana na matumizi ya dawa hizo. 

"Na hawa wana kikundi chao wanafanya shughuli zao hivyo hata wakikopeshwa wana uwezo mzuri wa kurudisha kwani kikundi chao kiko makini na wanajitambua kwani baadhi yao ni wasomi wazuri na wana uwezo mkubwa wanashindwa kukopesheka kama vijana kwani wengi wana umri mkubwa,"amesema Kilonzo.


HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YAIKOSHA KAMATI YA BUNGE KWA UBORA WA HUDUMA

 


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI imeipongeza menejimenti na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa kwa ubora wa Huduma na kuwatia moyo kwa  kuendelea kuwahudumia wananchi .

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI, Mhe. Stanslaus Nyongo baada ya kupokea taarifa ya Huduma za kibingwa na bingwa bobezi zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa iliyopo Jijini Dodoma.

Mhe. Nyongo amesema kuwa Hospitali hiyo imekuwa ya mfano katika utoaji wa Huduma bora na  usafi wa mazingira na kuleta ufanisi sahihi wa uwekezaji mkubwa ulofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Sluhu Hassan.

“Hongereni kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuwahudumia watanzania lakini pia Mkurugenzi husisite kutuma kutuma vijana wako kuendelea kujifunza ili Tanzania tuzidi kuwa kivutio cha tiba Utalii Afrika mashariki na Afrika nzima kwa ujumla”, Amesema Mhe. Nyongo.

Vile vile ametoa wito kwa uongozi huo kwendelea kuwa wabunifu katika kuongeza mapato ya hospitali hiyo ili kujiimarisha zaidi kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi kwa serikali kuu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa, Dkt. Alphonce Chandika ameishukuru serikali chini ya uongozi imara wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika Hospitali hiyo hususani katika vifaa tiba na vitendanishi, kusomesha wataalamu na upatikanaji wa dawa kwa wakati.

Saturday, February 3, 2024

TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE YATEMBELEA BUNGENI




Taasisi ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani yatembelea Bungeni Tarehe 2.2.2024 Kwa Mwaliko wa Mhe Subira Mgalu Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Kwa lengo la Kujifunza Shughuli za Bungeni.

Katibu wa Taasisi hiyo Mkoa wa Pwani Ndugu Omary Punzi Kwa niaba ya Taasisi alitoa Shukrani Kwa Mbunge Subira Mgalu Kwa namna alivyoipokea Taasisi na kuheshimu sambamba na hilo alipongeza Juhudi za Serikalini ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassani namna Bunge lilivyokuwa linafanya kazi Vizuri Kwa uchangamfu sana na Kujibu hoja vizuri

Thursday, February 1, 2024

AMEND TANZANIA LATOA MAFUNZO KWA MAOFISA USAFIRISHAJI.



Shirika la AMEND Tanzania ambalo linajihusisha na masuala ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usalama barabarani limeweza kutoa elimu na mafunzo kwa maafisa wasafirishaji wa vituo tofauti katika jiji la Dodoma.

Shirika hilo ambalo lipo chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania limeweza kutoa elimu na mafunzo kwa maafisa wasafirishaji maarufu kwa jina la bodaboda kwa malengo ya kudhibiti wigo ajali barabarani pamoja na kuwapa mafunzo mbali mbali pamoja na utumiaji wa alama za barabarani ambazo zimekuwa zikipuuzwa na maafisa wasafirishaji hao.

Nuhu Toyi ambaye ni balozi wa mafunzo na afisa msafirishaji kutoka kituo cha UDOM  jijini Dodoma amesema alibaatika kupata mafunzo ambayo yametolewa na shirika la AMEND Tanzania na kupitia mafunzo hayo yameweza kumsaidia kuendesha chombo chake kwa kujihamini bila kusababisha ajali.

“Pongezi za dhati ziende kwa Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania hususan kitengo cha afya kinachofadhiliwa na miss Vivian kwa kutambua umuhimu wa kundi hili la vijana wa bodaboda wengi ni vijana ambao tupo kati ya umri wa miaka 25. Kazi hii wengi tumekuwa tukiifanya kwa mazoea na hatuna elimu kwaio wengi tumekuwa ni wahanga wa kusababisha au kusababishiwa ajari kwasababu ya kukosa elimu barabarani lakini Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania umeona itakuwa ni vyema kama vijana hawa ambao ni taifa la kesho na nguvu kazi ya taifa wasiweze kudhuulika na ajali” alisema Toyi.

Kwa upande wake afisa usafirishaji, Laurenti Mayowa amesema alikuwa haelewi alama za barabarani lakini kupitia mafunzo hayo wamepokea kutoka shirika la AMEND Tanzania kwani limekuja kitofauti katika kutoa mafunzo yao kwani wamefundishwa kwa nadharia pamoja na vitendo.

“Tulipata mafunzo mazuri sana kwenye swala la uendeshaji wa pikipiki lakini pia tumeweza kufundishwa namna ya kutumia barabara lakini pia namba ya kutumi vyombo vyetu, kwa kweli mafunzo yalikuwa mazuri nimejifunza mambo mengi na mazuri na kabla ya mafunzo nilikuwa sielewi kwamba barabarani nilikuwa naendesha hovyo hovyo tu na baada ya mafunzo nashukuru mpaka sasaivi nime elewa na tulikuwa wengi sana tukifundishwa awamu kwa awamu nafikiri bodaboda takriban 230 au 250 kwa Dodoma hapa na sasahivi wame elimika”, alisema Mayowa.

Alisema alama za barabarani ilikuwa ni changamoto kwa madereva wengi , walikuwa wanaziona lakini wanashindwa kuzitumia kama ipasavyo na walidhani ni michoro tu lakini baada ya mafunzo waliweza kuelewa aina za michoro na alama zinazotumiwa barabarani.

“Tulifundishwa kuna alama za onyo, alama za amri, kuna alama za maelekezo kwaio hayo yote tumefundishwa lakini pia nimefundishwa alama nyengine ambazo nilikuwa sizielewi vizuri kama alama za michoro juu ya sakafu ya barabara hizo nazo nilikuwa sizielewi nilikuwa naona tu michoro na sielewi maana yake lakini baada ya elimu nimevielewa vizuri” alisema Mayowa

Aidha alisisitiza kwa maafisa usafirishaji kubadilika  na kuwa na mahudhurio mazuri ya mafunzo yanayotolewa na shirika la AMEND Tanzania kwasababu yanafundishwa kwa vitendo pamoja na kutii sheria za barabarani.

“Tumefundishwa dereva kujihami kwaio wale ambao hawajapata mafunzo hawezi kuelewa na kutii sheria akiwa yupo barabarani na anaweza kusababisha ajali kwasababu anakuwa hana uelewa wowote na vigumu kujilinda anapotumia chombo chake”,Mayowa.

Naye afisa usafirishaji kutoka kituo cha Ndasha,Bw. Ally Rashid Ally alisema kuwa bodaboda ni ajira kama zilivyo ajira nyengine na imeteka soko kubwa la ajira kwa vijana kwenye upataji wa kipato na awali haikupewa thamani kama zilivyo biashara nyengine.

Amesema wamekuwa na madereva usafirishaji wengi lakini baadhi yao kwenye kundi hilo hawana elimu ya kutosha ya barabarani na kutambua alama zilizomo.

Aidha Bw. Ally amesema elimu iliyotewa ni msaada mkubwa kwa maafisa usafirishaji mkoani Dodoma kwani wengi wao wamekuwa na nidhamu iwapo wanatumia vyombo vyao barabarani na changamoto za ajali na vifo vimeweza kuepukika kutokana na maarifa waliopokea kutoka kwa wakufunzi kupitia shirika la AMEND Tanzania.