HUKU Serikali ikiendelea na mchakato wa namna ya utoaji mikopo ya asilimia 10 za Halmashauri imeombwa kuangalia namna ya kuvikopesha vikundi vya waraibu wa dawa za kulevya ili wafanye shughuli za ujasiriamali.
Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Yohana Kilonzo Mkurugenzi wa Taasisi ya (OYARB) inayowahudumia watu waliokuwa wakitumia dawa za kulevya na kuacha na sasa wanatumia dawa za Methadoni zinazosaidia kuwarudisha katika hali yao ya kawaida ambapo kituo hicho kina vijana 500.
Kilonzo amesema kuwa watumiaji hao wanapokuwa hawana shughuli ya kufanya ni rahisi kurudia kutumia dawa za kulevya hivyo kuna haja ya kuwapatia shughuli za kufanya ili waweze kujipatia kipato.
"Wakati wakiendelea na tiba tunawafundisha shughuli za ujasiriamali ambapo wana mradi wa uuzaji wa sabuni za maji lengo wakitoka hatua hii wawe na uwezo wa kujitegemea ndiyo sababu tunaona nao wafikiriwe kwenye hiyo mikopo wapewe upendeleo,"amesema Kilonzo
Amesema kuwa kwa baadhi ya waliofuzu tiba hiyo baada ya kutumia Methadoni kwa kipindi cha miaka miwili ambazo wanapewa Hospitali ya Mkoa ya Rufaa ya Tumbi wamewachukua na kazi yao ni kufundisha juu ya athari na kuachana na matumizi ya dawa hizo.
"Na hawa wana kikundi chao wanafanya shughuli zao hivyo hata wakikopeshwa wana uwezo mzuri wa kurudisha kwani kikundi chao kiko makini na wanajitambua kwani baadhi yao ni wasomi wazuri na wana uwezo mkubwa wanashindwa kukopesheka kama vijana kwani wengi wana umri mkubwa,"amesema Kilonzo.
No comments:
Post a Comment