Tuesday, February 20, 2024

MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA KUENDELEA KUWEZESHWA

 


NA WELLU MTAKI, DODOMA

Serikali inaendelea kuiwezesha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ikiwa ni pamoja na kuboresha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ili kuongeza kasi ya mapambano na hatimaye kumaliza kabisa tatizo la dawa za kulevya nchini. 

Hayo yamesemwa na waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu sera bunge na uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya serikali Katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa Mwaka 2023

Amesema Serikali imepata mafanikio makubwa ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Disemba 2023 Zaidi kilogramu milioni 1 za aina mbalimbali za dawa za kulevya zilikamatwa katika maeneo mbalimbali nchini huku Watuhumiwa 10,522 ambao kati yao wanaume ni 9,701 na wananwake ni 821 walikamatwa kuhusika na dawa hizo.

"Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti Kupambana na Dawa za Kulevya imepata mafanikio makubwa ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Disemba 2023 kilogramu 1,965,340.52 za aina mbalimbali za dawa za kulevya zilikamatwa katika maeneo mbalimbali nchini. Watuhumiwa 10,522 ambao kati yao wanaume ni 9,701 na wananwake ni 821 walikamatwa kuhusika na dawa hizo. Aidha, jumla ya hekari 2,924 za mashamba ya bangi na mirungi ziliteketezwa" amesema Mhagama.

Aidha amesema kuwa Serikali imefanikiwa kuzuia uingizaji wa zaidi kilogramu milioni 15 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya kinyume cha sheria.

"Kiasi cha dawa za kulevya kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja pekee ni kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa hapa nchini kwani kinazidi kiasi cha kilogramu 660,465 zilichokamatwa katika kipindi cha miaka 11. Aidha, Serikali imefanikiwa kuzuia uingizaji wa kilogramu 157,738.55 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya kinyume cha sheria" amesema Mhagama.

Pia ameeleza kuwa kumekuwepo na ongezeko la waraibu wanaojiunga na tiba katika kliniki mbalimbali zilizopo nchini ongezeko hilo ni sababu ya kuadimika kwa dawa za kulevya mtaani baada ya kuvunja baadhi ya mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za  Kulevya imesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutoa elimu ya dawa za kulevya na rushwa kupitia klabu za kupinga rushwa nchini ambapo sasa zitaitwa  klabu za kupinga rushwa na dawa za kulevya. 




No comments:

Post a Comment