WATANZANIA wametakiwa kuenzi falsafa za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere za Ujamaa na Kujitegemea kwani siyo umaskini bali ni kuwafanya wananchi kuwa na umoja ili kujiletea maendeleo.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Taifa Paul Kimiti wakati wa Kongamano la Maadili lililofanyika kwenye Shirika la (TATC) Nyumbu Kibaha.
Kimiti alisema kuwa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema kuwa taasisi hiyo ilianzishwa ili kuyaenzi yale aliyoyafanya hasa katika kujitegemea.
"Sisi ambao tunajua alichokuwa akikitaka Nyerere kuhusu uzalendo na kujitegemea na kudumisha umoja na amani lazima tuwakumbushe viongozi na vijana ili wazingatie falsafa hizo ili kuleta maendeleo,"alisema Kimiti.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Nyumbu na Mkurugenzi wa Nyumbu Kanali Charles Kalambo alisema Shirika hilo ambalo ni maono ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere limepata mafanikio ikiwa ni pamoja na kubuni gari aina ya Nyumbu.
Kalambo alisema kuwa wanamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kulipatia Shirika la Nyumbu fedha kwa ajili ya kufanya shughuli zake mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendeleza miradi ya kiufundi.
Naye Kanali Ngemela Lubinga katibu mkuu mstaafu (NEC-CCM) siasa na uhusiano wa kimataifa akifundisha somo la uzalendo, itifaki na uadilifu alisema kuwa viongozi wanapaswa kuwa na moyo wa kujituma kwani ndiyo msingi wa kujenga jamii bora na yenye uzalendo.
Lubinga alisema kuwa viongozi wanapaswa kuwa na uadilifu ili kujenga jamii bora pia wawe wabunifu, moyo wa kujituma ili kuleta maendeleo kwa wananchi na awajali ili kuwa na mipango ya pamoja.
Balozi Mstaafu Meja Jenerali Anselm Bahati alisema kuwa ili kuwa na usalama mahali pa kazi kwa wafanyakazi lazima wafanyakazi wapate mafunzo ya namna ya kujilinda na kujikinga.
Bahati alisema kuwa wafanyakazi wakiwa na mazingira salama watakuwa na uwezo wa kuzalisha pia maslahi yao kuangaliwa ili kuepukana na afya ya akili inayotokana na msongo wa mawazo.
Naibu Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo Neema Mkwachu alisema malengo ni kutoa elimu kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi vyuo juu ya falsafa za Nyerere ikiwemo uzalendo wa nchi.
Mkwachu alisema kuwa pia ni kuwa na klabu za Mwalimu Nyerere ambazo zitakuwa zinatakuwa pia na uwezo wa kutunza mazingira ambayo ni moja ya vitu alivyohimiza Hayati Nyerere
Katibu wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Pwani Abdul Punzi alisema kuwa ili kuenzi falsafa za Nyerere kwa kufungua Klabu ya Mwalimu Nyerere Nyumbu.
Punzi alisema kuwa uzalendo unapaswa kuanzia chini kabisa ili wananchi watambue misingi mizuri iliyoasisiwa na Nyerere na kuifanya Tanzania kuwa na umoja na mshikamano ambapo kongamano hilo lilidhaminiwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Benki ya CRDB na NSSF.
No comments:
Post a Comment