Friday, February 23, 2024

SERIKALI KUENDELEA KUDHIBITI DAWA ZA KULEVYA NA RUSHWA



NA WELLU MTAKI , DODOMA.

SERIKALI inaendelea kukabiliana na masuala ya  biashara ya dawa za kulevya na rushwa nchini  ili kuhakikisha wanajenga taifa lililo imara kwa kutoa Elimu kuanzia shule za msingi mpaka vyuo vikuu.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya  Aretas Lyimo Jijini Dodoma   wakati  akifunga mafunzo kuhusu mkakati  wa habari , Elimu , mawasiliano  na programu ya TAKUKURU rafiki pamoja na  tatizo za dawa za kulevya , mapambano dhidi ya rushwa kwa maafisa wanaohusika na uelimishaji umma na mawasiliano.    

Lyimo amesema kupitia mafunzo waliopewa maafisa wanaohusika na uelimishaji umma na mawasiliano yatasaidia kuleta matokeo chanya ya  kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya na Rushwa kwani ni vitu vinavyofanana.

“Naamini kupitia muunganiko wetu na klabu ambazo tayari tumeshanzianzisha huko mashuleni itasaidia kuwafikia kwa uharaka zaidi watu katika ngazi za mitaa hadi huko kwenye Halmashauri  wanafunzi wengi wanatokea kwani huko,”amesema. Lyimo

Amesema matunda ya ushirikiano kati ya TAKUKURU na taasisi ya kupambana dawa za kulevya tayari yameanza kuonekana kwani vitu hivyo vimekuwa vikiisumbua serikali katika kuhakikisha wote wanao husika wanatiwa mbaroni na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Nitoe wito kwa wadau kuwa nyenzo pekee ya kuepusha watu kujiingiza kwenye Rushwa na dawa za kulevya ni kutoa elimu hata tukiendelea kukamata kwa namna gani lazima tuhakikishe tunatoa elimu pamoja na kushirikiana na vyombo vya habari ili watusaidie kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja,”amesema.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu TAKUKURU Bi. Neema Mwakalile amesema kilichotokea kwenye mafunzo hayo kinadhihirisha ushirikiano  uliopo kati ya TAKUKURU na Mamlaka ya Kupambana na dawa za Kulevya ni mkubwa kwani vitu hivyo vinafanana na mapambano yanapaswa kuimarishwa zaidi.

Mwakalile amesema kuwa washiriki wamejifunza juu ya tatizo la dawa za kulevya, sababu za matumizi ya dawa hizo pamoja na kutambua dawa tiba ambapo vijana wengi wameonekana kujiingizia kwa kiasi kikubwa katika janga hilo huku akiongeza kuwa elimu waliyo wapatia washiriki katika mkutano huo itaenda kuumarisha zaidi mapambano na hatimaye kufikia hazma ya Serikali.

“Washiriki walipitishwa kwenye mkakati wa kupambana na Rushwa ili kuelewa zaidi na namna ya kwenda kuelimisha wanafunzi pia mafunzo haya yatasaidia jamii kuichukia Rushwa na kuepukana na Dawa za kulevya,”amesema.Mwakalile

Pia ameongeza kuwa katika mambo mengi waliyowafundisha wataenda kutoa elimu hasa kwa wanafunzi kwani swala hilo limekuwa mtambuka. 

 “Ni lazima kuanza kuwajenga wanafunzi wa shule msingi na sekondari kwani wao ndio watakuwa msingi mzuri kwenda kupinga na kukataa dawa za kulevya pia  Rushwa na dawa za kulevya vina madhara makubwa kwenye nyanja zote elimu na uchumi,”ameongeza.

Taasisi ya kupambana na Rushwa na TAKUKURU waliingia makubaliano 20/5 2023 kwaajili ya kutoa elimu kuhusu rushwa na dawa za kulevya.

No comments:

Post a Comment