Monday, February 5, 2024

LATRA YACHUKUA HATUA KWA DALADALA ZINAZOKIUKA TARATIBU ZA USAFIRISHAJI/KUKATISHA RUTI

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Pwani imeyachukulia hatua za kisheria mabasi madogo Daladala 53 kutokana na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukatisha safari.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na ofisa leseni na usajili wa Mamlaka hiyo Geofrey Mashishi alipozungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake.

Mashishi amesema kuwa hatua hizo zimechukuliwa kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita Desemba mwaka jana na Januari mwaka huu kwa Daladala zinazofanya safari ndani ya Mkoa huo.

"Hatua hizo tumezichukuwa kwa wasafirishaji hao kwa sababu ya kukiuka masharti ya leseni zao kwa makosa mbalimbali mengine yakiwa ni kutotoa tiketi, kuzidisha nauli na mengine ambayo ni kinyume na taratibu za usafirishaji,"amesema Mashishi.

Amesema kuwa ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wasafirishaji wanaokiuka masharti ya leseni zao kunahitajika ushirikiano baina yao na wadau wakiwemo abiria.

"Sekta ya usafirishaji ina changamoto nyingi na tumekuwa tukifanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa kwashirikiana na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha wasafirishaji wanafuata kanuni, sheria na taratibu za usafirishaji ili kuondoa malalamiko,"amesema Mashishi.

Aidha amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa abiria ili kujua haki zao na wasafirishaji kujua wajibu wao wanapotekeleza majukumu yao kupitia vyombo vya habari.

"Ukaguzi wa kufuatilia ni endelevu hivyo ni vema wasafirishaji wakazingatia masharti ya leseni zao ili kuondoa changamoto zisizo za lazima kwa wadau wa usafiri,"amesema Mashishi.




No comments:

Post a Comment