MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ametoa fedha na vifaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi milioni 1.7 kwa ajili ya washindi wa Kombe la Kibaha Vijana Cup.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa uongozi wa Chama Cha Soka Kibaha (KIBAFA) ofisini kwake kwa niaba ya Mbunge huyo Katibu wa Mbunge Method Mselewa amesema fedha hizo na vifaa hivyo vitatolewa kwenye hatua ya fainali itakayochezwa Februari 21 kwenye uwanja wa Mwendapole.
Koka akizungumza kwa njia ya simu amesema kuwa ameamua kujitolea ili kuinua vipaji vya vijana wa Kibaha kwani michezo ni ajira kubwa kwa vijana na wengi wamenufaika kupitia soka na kuwa ni sehemu ya maendeleo.
Amesema kuwa ataendelea kusaidia michezo mbalimbali ili vijana wapate fursa kwenye timu kubwa ambapo chimbuko huanzia chini ambako ndiyo kwenye msingi.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa KIBAFA David Mramba amesema kuwa wanamshukuru mbunge huyo kwa kuchochea sekta ya michezo kwenye Jimbo hilo na kuwafanya vijana kushiriki michezo.
Naye Mjumbe wa soka la wanawake kupitia chama hicho Jesca Sihha amesema kutolewa zawadi hizo ni chachu kwa wanasoka na kuomba na soka la wanawake nalo lipewe kipaumbele.
No comments:
Post a Comment