Monday, February 5, 2024

MWENDAPOLE B KUJENGA SHULE YA MSINGI


MTAA wa Mwendapole B Wilayani Kibaha uko kwenye hatua za mwisho katika kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi ili kuwapunguzia changamoto watoto wa mtaa huo kugongwa na magari wakivuka kwenda shule iliyoko mtaa jirani.

Aidha wanafunzi wanaotoka mtaa huo hutembea umbali wa kilometa mbili kwenda na kurudi hivyo kuwa na uhitaji wa shule ili kuwapunguzia umbali mrefu kwenda shule.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha Mwenyekiti wa Mtaa huo Abubakary Matumla amesema kuwa mtaa huo una shule za msingi na sekondari za watu binafsi ambazo ni wazazi wachache wenye uwezo wa kuwapeleka watoto wao kusoma hapo.

"Tayari eneo limepatikana lina ukubwa wa hekari nne ambalo ni la mtu binafsi ambaye inabidi alipwe ndipo aliachie hivyo kuna makubaliano na Halmashauri ya Mji wampatie eneo lingine ili apishe hapo tuko hatua za mwisho za mabadilishano,"amesema Matumla.

Matumla amesema kuwa tayari wana tofali zaidi ya 4,000 kwa ajili ya ujenzi huo hivyo wanasubiri tu Halmashauri wampatie eneo lingine ili waanze ujenzi wa shule hiyo ambayo itawaondolea changamoto ya kugongwa au kusoma mbali.

"Wananchi wameshachanga fedha kiasi cha shilingi milioni 1.6 ambapo tunashirikiana na diwani ili kufanikisha kupata eneo hilo na matumaini ni makubwa,"amesema Matumla.

No comments:

Post a Comment