Friday, February 23, 2024

KIJANA WA KITANZANIA AGUNDUA MFUMO WA KITAALUMA KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA MSINGI HADI CHUO KIKUU

NA WELLU MTAKI Dodoma.

KIJANA wa Kitanzania Alpha Mbennah mwenye taaluma ya Uhandisi amegundua Mfumo wa Uchakataji,Uhifadhi na Uandaaji wa Taarifa za Kitaaluma za wanafunzi kuanzia ngazi ya Elimu msingi mpaka Vyuo Vikuu uitwao "SPIN-ED Academic Performance Management System utakaowezesha kuleta ufanisi katika kazi.

Akizindua mfumo huo  Jijini Dodoma katika Mkutano wake na Wanahabari Mhandisi Mbennah amesema kuwa mfumo huo unamruhusu mwalimu katika ngazi tajwa kuweza kukusanya na kuingiza alama za mwanafunzi aliyesajiliwa katika mfumo kisha huchukua alama hizo na kuzichakata kwa kutengeneza wastani uliopimwa au usiopimwa kubaini gredi ya alama hizo, yaani A, B, C, n.k.

“Pia huu mfumo unaweza kubaini wastani wa darasa husika, nafasi aliyoshika kila mwanafunzi katika somo husika na katika darasa kwa ujumla pamoja na kutengenza ripoti ya maendeleo ya kitaalamu kwa kila mwanafunzi aliyesajiliwa kwenye mfumo, katika darasa husika, kutoa maoni ama comments zinazohusiana na ufaulu wa mwanafunzi na kuchora grafu ya maendeleo ya kitaaluma kwa kila mwanafunzi".

Mbenah amesema kuwa vyote hivyo hufanywa moja kwa moja huku akisema kuwa hivo ni baadhi ya vipengele vilivyopo katika mfumo wa SPIN-ED.

“Niseme tu kwamba vina umuhimu mkubwa sana katika uchakataji wa taarifa za kitaaluma za wanafunzi kwani huwasaidia walimu na wadau mbalimbali wa elimu kufanya maamuzi mbalimbali na hatimae kuongeza ufanisi katika mbinu za ufundishaji na ujifunzaji".

Aidha amesema sababu kubwa ya yeye kufanya ugunduzi wa mfumo huu wa SPIN-ED ni kutokana na changamoto alizoziona wakati akiwa mwalimu wa kujitolea katika moja ya shule hapa nchini, hususan katika uandaaji wa ripoti za maendeleo ya kitaaluma ya wanafunzi.

wakati mwingine huchukua muda mrefu kwa Walimu kuandaa na hata wakati mwingine Walimu kukosa hamasa ya kutoa majaribio ya mitihani ya Mara kwa Mara ya kuwapima wanafunzi wakihofia kuchukua muda kwa uandaaji wa ripoti na Maendeleo yao.

Mfumo huu wa SPIN-ED ameugundua mwaka 2021 na kuanza kufanya kazi mwaka huohuo ambapo mpaka kufika sasa zipo shule 3 zinazotumia mfumo huu.

No comments:

Post a Comment