Akizungumza na wananchi wa Mtaa huo Diwani wa Kata ya hiyo Ramadhan Lutambi alisema kuwa hiyo ni fursa kwa wananchi kuelekea kupata umiliki wa ardhi kisheria.
Lutambi alisema kuwa kumiliki ardhi kisheria kuna faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuepukana na migogoro ya ardhi ambaye imeleta changamoto kubwa kwa wananchi.
"Tunaishukuru Serikali kwa kupunguza gharama za urasimishaji ardhi hivyo kuwafanya wananchi kumiliki ardhi kisheria hivyo kuwa na umiliki halali na kupunguza migogoro,"alisema Lutambi.
Akizungumzia suala la changamoto ya maji alisema kuwa kuna mradi wa maji ambao kwa sasa uko kwenye utekelezaji ambapo mitaa yote itapitiwa ambapo kwenye mtaa huo watu zaidi ya 8,000 hawapati huduma hiyo.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo alisema kuwa mikopo ya asilimia 10 ipo kwa makundi wakiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Mawazo alisema kuwa fedha zimetengwa jambo kubwa ni walengwa kuunda vikundi ambavyo vitatimiza masharti ikiwa ni pamoja na usajili huku kwa watu wenye ulemavu hata kwa mtu mmoja anaruhusiwa.
Akizungumza kwa njia ya simu Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John alisema kuwa mradi wa maji wa Pangani utaondoa changamoto ya maji kwenye mtaa huo hivyo wananchi wawe na subira.
John alisema kuwa Serikali imekuwa ikipambana kuhakikisha wananchi wanaondokana na changamoto hiyo ambayo imekuwa kero kubwa lakini inakwenda kupatiwa suluhu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa alisema kuwa mipango iliyopo ni ujenzi wa Shule ya Sekondari na Zahanati.
Shemwelekwa alisema kuwa kuhusu urasimishaji vifaa vimenunuliwa kwa ajili ya urasimishaji hivyo wananchi wajiandae na watazichukua changamoto zilizotolewa na wananchi ili wazipatie ufumbuzi.

No comments:
Post a Comment