MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo amekabidhi mashine ya kudurusu karatasi kwa Shule ya Sekondari Mwambisi na kusema kuwa itapunguza gharama za uandaaji mitihani.
Mawazo alikabidhi mashine kwa uongozi wa shule hiyo kwa kushuhudiwa na Ofisa elimu Sekondari, bodi za Shule za Sekondari za Manispaa, baadhi ya wazazi na wanafunzi wa Shule hiyo.
Amesema kuwa Serika inaendelea kuwaka mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi ili kuongeza ufaulu na kupunguza changamoto za Shule ndani ya Manispaa.
"Utoaji wa mashine hii ni kuunga mkono jitihada za Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa elimu kwani amejitahidi kujenga miundombinu ya elimu,"amesema Mawazo.
Aidha amesema kuwa miaka ya nyuma Shule zilijengwa na wananchi lakini kwa miaka ya sasa Serikali imejenga miundombinu mingi ya elimu hivyo wadau nao waunge mkono serikali.
"Kuhusu bweni wenyeviti wa bodi za Shule zielezee kwenye mipango yao juu ya mahitaji hayo na kama yapo tutaongea na wadau ili kushirikiana na serikali kuyajenga kama kuna mahitaji hayo,"amesema Mawazo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Yahaya Mtonda amesema kuwa kuna haja ya kuipandisha hadhi Shule hiyo ili iwe na kidato cha tano.
Mtonda amesema kuwa baadhi ya wanafunzi wanashindwa kwenda kusoma mbali pale wanapofaulu kutoka Shule za Msingi kwenye Manispaa ya Kibaha.


No comments:
Post a Comment