Monday, September 28, 2026

VIWANDA ZEGERENI VYA HITAJI LAMI KUKABILIANA NA MVUA

KIWANDA cha King Lion Steel kimeiomba serikali kuweka lami kwenye barabara inayoelekea viwandani ili kukabiliana na ubovu wa barabara hasa kipindi cha mvua.

Akizungumza na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha ambaye alifanya ziara kutembelea maeneo ya uwekezaji wa viwanda kuangalia namna ya kukabiliana na mvua za Elnino Meneja Mkuu wa kiwanda hicho Kelvin Richard alisema kuwa barabara ni changamoto kubwa.

Richard alisema kuwa wamekuwa wakimwaga vifusi ili barabara ipitike lakini inapofika kipindi cha mvua magari kupita ni mtihani kwani kuna kuwa na tope na kuyafanya magari hayo kukwama.

"Kwa kuwa barabara hii inaelekea kwenye viwanda ni vizuri ikawekwa lami badala ya kuchonga kwani hilo ndiyo litakuwa suluhisho la barabara hiyo yenye urefu wa kilometa mbili,"alisema Richard.

Alisema kuwa barabara hiyo inaelekea kwenye viwanda tisa hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuwekewa lami ili kukabili changamoto hiyo hasa ikizingatiwa malori yanaingia kupeleka malighafi au bidhaa baada ya kuzalishwa.

Akijibu hoja hiyo Meya wa Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo alisema kuwa serikali imeweka mipango mizuri ili kuhakikisha wawekezaji hawapati changamoto ya miundombinu na masuala mbalimbali ili kurahisisha utendaji kazi.

Mawazo alisema kuwa katika kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji Manispaa ya Kibaha ilitenga eneo la Zegereni kuwa la uwekezaji wa viwanda kwa kuweka miundombinu rafiki ikiwemo barabara za lami, umeme, maji na mawasiliano.

Aliwataka wenye viwanda kuchukua tahadhari wakati wa mvua za Elnino ili wasikwame katika uzalishaji wa bidhaa wakati huo wa mvua zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Kwa upande wake Mhandisi kutoka Tarura Collins Mrashani alisema kuwa tayari barabara hiyo imeshaombwe fedha kwa ajili ya kuwekewa lami ili kuondokana na changamoto hiyo.

Mrashani alisema wamelipa kipaumbele eneo hilo kutokana na umuhimu wake kwani kuna viwanda tisa ambavyo vinatumia barabara hiyo hivyo uhitaji wa lami ni mkubwa.

No comments:

Post a Comment