KUFUATIA ombi la Shule nyingi za Sekondari za kutwa kuomba kujengewa mabweni kwa ajili ya wanafunzi Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo amesema kuwa atapeleka pendekezo hilo kwenye Baraza la Madiwani ili kuweka mpango huo.
Mawazo ameyasema hayo kwenye Shule ya Sekondari ya kutwa ya Misugusugu wakati wa ziara yake kukagua miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu na barabara na viwanda ili kujua changamoto zilizopo kwenye sekta hizo.
Amesema kuwa ametembelea Shule nyingi za Sekondari lakini zote maombi yao makubwa ni kujengewa bweni kwa ajili ya wanafunzi wa Shule hizo.
"Nimekuja hapa Misugusugu na kabla kuja hapa nimetembelea Sekondari nyingi lakini zote hilo ni ombi lao kubwa kwa hiyo kuna haja ya kupeleka maombi haya kwenye Baraza la Madiwani ili liwe azimio,"amesema Mawazo
Aidha amesema kuwa kama hili ndilo hitaji na ni kipaumbele basi mpango uwekwe ili waanze ujenzi wa mabweni kwa Shule kujengewa mabweni kwa ajili ya wanafunzi.
"Kuna baadhi ya Shule kweli zina uhitaji wa mabweni kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo umbali hivyo kuna haja ya kujengwa mabweni mfano hapo jirani na Shule hiyo kuna sehemu ya kulaza malori hali ambayo ni hatari hasa kwa wanafunzi wa kike,"amesema Mawazo.
Naye Diwani wa Viti Maalum Sara Uledi amesema kuwa asilimia kubwa ya wanafunzi wanaosoma Shule ya Sekondari Misugusugu wanaishi na mzazi mmoja.
Uledi amesema kuwa wanafunzi wengine wanaishi mbali na Shule hivyo kuwa na changamoto ya umbali kutoka nyumbani hadi Shuleni na kurudi pi
Kwa upande wake Ofisa Elimu Sekondari Theresia Charles amesema kuwa kuna uhitaji wa mabweni kwa baadhi ya Shule kutokana na mazingira ya baadhi ya wanafunzi.
Charles amesema kuwa kuhusu umbali sheria inataka wanafunzi wasitembee umbali wa zaidi ya kilometa saba pia Shule ambazo zina mabweni zinafanya vizuri.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Misugusugu Mohamed Lacha amesema kuwa baadhi ya changamoto ni ukosefu wa mabweni na uzio wa Shule.
Lacha amesema kuwa pia wanahitaji huduma ya maji na umeme ambapo tayari wako kwenye hatua mbalimbali za kupata huduma hizo lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa fedha.
mwisho.

No comments:
Post a Comment