Na John Gagarini, Kibaha
MARAFIKI wa Simba (Friends of Simba) wametakiwa kuingilia
kati tatizo lililopo kwenye klabu yao ili iweze kuwa na mwenendo mzuri katika mashindano
mbalimbali inayoshiriki timu yao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi msemaji wa tawi la
Simba wilayani Kibaha “Simba Tishio” Fahim Lardhi alisema kuwa hadi sasa timu
hiyo bado haijapata tiba ya tatizo lililopo ndani ya klabu hiyo.
Lardhi alisema kuwa wakati huu wa matatizo wanachama na wadau
wa Simba lazima wajitokeze kusaidia timu ili iweze kufanya vema kwani kwa sasa
mwenendo wake ni mbaya.
“Marafiki wazuri huonekana wakati wa shida hivyo tunataka
marafiki wetu wajitokeze kuinusuru timu kwani kwa sasa timu inaonekana kufanya
vibaya kwenye michezo yake tofauti na matarajio ya wengi,” alisema Lardhi.
Alisema kuwa marafiki wa Simba mbali ya kusaidia fedha pia
wanatakiwa kuisaidia timu hiyo kwa mchango wa mawazo ili kujua tatizo lililopo
hadi timu kufanya vibaya kwenye michezo yake.
“Wanapaswa kuonyesha upendo wao kwa klabu kwani hadi sasa
hatujaona jitihada zozote walizofanya kuinusuru timu na matokeo mabaya,
tunawpongeza wanaposaidia timu katika mazingira yote pia waonyeshe upendo hata
kama timu inafanya vibaya ili kuinusuru timu yetu ambayo inatetea ubingwa wake
wa ligi kuu ya Tanzania Bara,” alisema Lardhi.
Msemaji huyo wa tawi la Simba wilayani Kibaha alisema kuwa
Wanasimba wanatakiwa kuungana katika kipindi hichi kigumu kinachoikabili timu
yao kwa kuwa na matokeo mabaya inayoyapata ili kujinusuru na kupata matokeo
mazuri.
“Tunapaswa kuungana na kuonyesha mshikamano ili kuisaidia
timu yetu kwani timu inapofanya vibaya tunaumia sana hivyo tuungane ili
kuiletea maendeleo mazuri,” alisema Lardhi.
Ameipongeza kamati ya utendaji kwa kuandaa mkutano wa kujadili
kiini cha timu kufanya vibaya katika michezo yake hali ambayo inaifanya timu
hiyo kuwa kwenye mashaka ya kutetea ubingwa wake.
Mwisho.