Monday, April 18, 2016

KILUA YAUNGA MKONO DHAMIRA YA DK MAGUFULI KUJENGA VIWANDA

Na John Gagarini, Kibaha
KATIKA kuunga mkono dhamira ya Rais Dk John Magufuli ya uchumi wa nchi kutegemea viwanda kampuni ya Kilua Steel inatarajia kuanza uzalishaji wa bidhaa za vyuma zikiwemo nondo pamoja na vyuma mbalimbali ifikapo mwezi Mei mwaka huu.
Uzalishaji wa vyuma kwenye kiwanda hicho utapunguza bei ya bidhaa za vyuma kwa asilimia 25 ya bidhaa hizo ambazo nyingi zinaagizwa toka nje ya nchi hivyo kuongeza mapato ya ndani.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kiwanda hicho kilichopo Kitongoji cha Disunyala Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani mkurugenzi wa kiwanda hicho Mohamed Kilua alisema kuwa kiko kwenye hatua za mwisho za kuunganisha umeme mkubwa wa viwandani kwani uliopo ni mdogo na hauwezi kuendesha mashine za kiwanda hicho.
Kilua alisema kuwa kiwanda hicho ambacho kitakuwa ni cha kipekee hapa nchini na barani Afrika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.5 kwa mwaka huku kwa siku kikitarajiwa kuzalisha tani 2,000 kwa awamu ya kwanza na kufikia tani 7,000 itakapofikia awamu ya tatu na itatoa ajira kwa watu zaidi ya 2,000.
“Tunatarajia kuzalisha vyuma vyenye ubora wa kimataifa ili viweze kuwa na soko sehemu yoyote ile duniani kwani tuna wataalamu kutoka nchi ya China ambao ndiyo tunaoshirikiana nao hapa,” alisema Kilua.
Alisema kuwa tayari malighafi za kutengenezea vyuma wanazo ambazo zinatoka nchi kama vile Brazil na nchi zinazotengeneza vyuma duniani lakini mara kitakapoanza kazi kitakuwa na malighafi zake.
“Tunarajia malighafi zote mara tutakapoanza uzalishaji zitapatikana hapa hapa hivyo bei ya vyuma itashuka na nchi itapata maendeleo kupitia kodi mbalimbali kwenye kiwanda,” alisemaKilua.
Aidha alisema kuwa vyuma vitakavyozalishwa hapo mbali ya nondo ni pamoja na vyuma vinavyo husika na ujenzi wa madaraja makubwa, mabomba yatakayotumia gesi, maghorofa kufikia urefu wa ghorofa 50 na kuendelea na vyuma vya engo tofautitofauti ambavyo vitapatikana na kuwapunguzia gharama wananchi katika shughuli zao zinazohitaji vyuma.
Kwa upande wake mkurunzi mwenza kutoka nchni China Wang Zuojin alisema kuwa aliamua kushirikiana na Kilua ikiwa ni moja ya njia za kuenzi urafiki wa nchi hizo ambao ulianzishwa na Mwalimu Julius Nyerere zaidi ya miaka 50 iliyopita.
Zuojin alisema kuwa nchi ya China miaka mingi iliyopita ya nyuma ilikuwa maskini lakini walijipanga hasa kupitia viwanda na kuifanya nchi hiyo kuwa yenye uchumi mkubwa duniani kupitia viwanda.
“Rais Dk John Magufuli ni mtu anayependa maendeleo na tumeamua kumuunga mkono kwa sera zake za kuinua uchumi wa wananchi wake kwa kuendeleza sekta ya viwanda ili kuwa na uchumi wa kati kwa kufanya mapinduzi ya viwanda,” alisema Zuojin.
Alisema kuwa anachokisema Dk Magufuli kinawezekana kwani hata China ilikuwa chini kiuchumi lakini walipoamua kuwekeza kwenye viwanda wamefanikiwa na kuwa nchi zenye uchumi mkubwa duniani na kuwaondoa wananchi wake kwenye umaskini.
Mwisho.
   





Friday, April 15, 2016

WATUMISHI HEWA WAITIA HASARA SERIKALI KIASI CHA SHILINGI MILIONI 641


Na John Gagarini, Kibaha

MKOA wa Pwani umebaini uwepo wa watumishi hewa 25 wakiwemo walio kufa na wameipa serikali hasara kiasi cha shilingi milioni 641,361,239 kutokana na kupokea mishahara pasipo kufanya kazi ambalo ni kosa kisheria.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mjini Kibaha mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evaristi Ndikilo alisema kuwa hasara hiyo imebainika baada ya kufanya uhakiki kwa mara ya pili na kuona kuwa fedha za mishahara ziliendelea kutolewa kwa watumishi hewa licha ya kutokuwepo kazini.

Ndikilo alisema kuwa kati ya watumishi 19 ni wale waliokufa, waliostaafu na kuacha kazi lakini mishahara yao ilikuwa ikiendelea kutoka na kusababisha hasara hiyo baada ya kuwafanyia uhakiki watumishi 150 ili kuwatafuta watumishi hewa kutokana na agizo la Rais Dk John Magufuli.

“Kundi hili la kwanza limeipa hasara serikali kiasi cha shilingi milioni 69.1 huku wale ambao hawapo kabisa kazini wameipa hasara serikali kiasi cha shilingi milioni 12.4 na watumishi watoro na wale walio na mashauri ya kinidhamu wameipa hasara serikali kiasi cha shilingi milioni 448.2,” alisema Ndikilo.

Alisema kuwa kati ya watumishi 150 waliohakikiwa 31 walibainika kuwa ni watoro na hawakujitokeza siku ya uhakiki lakini walionekana kuwa ni watumishi halali kwa kuonyesha nyaraka muhimu huku 18 wakibainika kuwa ni watoro na wanamashauri ya kinidhamu lakini waliendelea kulipwa mishahara.

“Watumishi 76 ambao ni watoro na wanamashauri ya kinidhamu mishahara yao imesimamishwa ili wasiendee kuitia hasara serikali wakati mashauri yao yanafanyiwa kazi,” alisema Ndikilo

Aidha alisema kuwa wakurugenzi wa Halmashauri saba za wilaya walisema kuwa kiasi cha shilingi milioni 249,452,390  zilirudishwa Hazina na kuwataka wapeleke viambatanisho kama ushahidi vinavyoonyesha kuwa walipeleka hazina na si maneno matupu.

“Kama ni kweli kiasi hicho cha fedha kilipelekwa hazina fedha ziltakazokuwa zimepotea ni kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 391.8 ambazo wanapaswa kuonyesha vielelezo vya kuzipeleka hazina kwani maelezo hayo bado hayajaturidhisha wanatakiwa watupe uthibitisho ili tuliamini hilo,” alisema Ndikilo.     


Mwisho.

Saturday, April 9, 2016

HOSPITALI YA BAGAMOYO YADAIWA M 220 NA MSD

Na John Gagarini, Kibaha
HOSPITALI ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani inakabiliwa na upungufu mkubwa wa dawa baada ya kukosa dawa kuanzia Januari mwaka huu kutoka Bohari Kuu ya Madawa (MSD) kutokana na kudaiwa deni la shilingi milioni 220.
Hayo yamesemwa na mganga mkuu mfawidhi wa Hospitali hiyo Tumaini Byron wakati Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo kutembelea wagonjwa na kuwapa misaada mablimbali katiaka kusherehekea miaka 61 ya kuanzishwa Jumuiya hiyo.
Dk Byron amesema kuwa kutokana na deni hilo Hospitali hiyo kwa sasa imeonekana haikopesheki kutokana na deni hilo hivyo kunywimwa dawa hadi pale watakapolipa deni hilo la madawa.
Amesema wanakosa dawa kutokana na deni hilo kwani hata wakiomba hawapati hivyo kuwapa wakati mgumu wao pamoja na wagonjwa ambao hutakiwa kwenda kununua kwenye maduka ya madawa.
Aidha amesema kuwa wanashindwa kupewa au kukopeshwa vifaa tiba pamoja na vipimo mbalimbali ikiwa ni pamoja na vipimo vya wingi wa damu mkojo na malaria.
Amebainisha kuwa changamoto nyingine ni upungufu wa watumishi kwani kwa sasa wana watumishi 147 huku mahitaji yakiwa ni watumishi 250, vitanda vilivyopo ni 24 tu ambapo walau vingepatika japo 100 pamoja na uchakavu wa miundombinu ya umeme..
Kwa upande wake Mfamasia wa wilaya ya Bagamoyo Mohamed Makarai amesema kuwa mbali ya deni hilo la dawa pia MSD kutokuwa na dawa hivyo kuwa ni tatizo la nchi nzima kuanzia Oktoba na Novemba mwaka jana.
Makarai amesema kuwa serikali ilibadilisha mfumo wa kutoa tenda kwa wazabuni kwa ajili ya kuwapelekea dawa ambapo kwa sasa utaratibu umebadilika kwani hakutakuwa na kutoa tenda tena.
Amesema kuwa walikuwa wakichukua dawa kwa mali kauli na kutoa fedha baadaye hata hivyo walitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 100 ambapo moja ya changamoto ya kukosa fedha ni pamoja na kuwa na misamaa ikiwemo ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wazee, wajawazito na wale wenye magonjwa sugu hivyo serikali inapaswa kufidia pengo la makundi hayo ambayo yanapewa dawa bure.
Mwisho.

Monday, April 4, 2016

UVCCM WATAKIWA KUTUMIA KILIMO KAMA FURSA NA SIO KAMA ADHABU

Na John  Gagarini, Kibaha
VIJANA wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi  CCM (UVCCM) wilayani Kibaha wametakiwa kukitumia kilimo kama moja ya chanzo cha kujikomboa kiuchumi kwani hiyo ni fursa na si adhabu.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa CCM (MNEC) Rugemalila Rutatina wakati akifungua mkutano wa Baraza la (UVCCM) Kibaha Mjini na kusema kuwa kilimo endapo kitatumia vizuri kinaweza kuboresha uchumi wao badala ya kumtegemea mtu kuwasaidia.
Rutatina alisema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakiwafanya vijana kama ngazi ya kupandia kwa kuwafanikishia mambo yao kisha kuwaacha bila ya kuwajengea mazingira endelevu.
“Uzuri ni kwamba Chama pamoja na umoja wenu una mashamba ambayo ni kama mtaji wa kuanzia kwa ajili ya kilimo cha kisasa ambacho kitakuwa na tija kwa kutumia mipango mbalimbaili ya kuendeleza kilimo ikiwa ni pamoja na Kilimo Kwanza,” alisema Rutatina.
Alisema kuwa ili vijana wajikomboe wanapaswa kuanzisha miradi ya kudumu kupitia rasilimali za chama ambazo endapo zingetumika ipasavyo zingewaondoa vijana ndani ya chama na nje kuwa tegemezi katika kuendesha umoja wao.
“Kilimo ni moja ya njia za kuwakomboa na kuacha kumtegemea mtu lakini endapo mtaanzisha miradi ya kilimo itawaondoa huko mliko na kuwafanya mjitegemee na kuendesha mambo yenu bila kuwa tegemezi,” alisema Rutatina.
Aidha alisema kuwa kwa sasa fursa ni nyingi kwa vijana ikiwa ni pamoja na mikopo kwa ajili kujikwamua kiuchumi na zana za kilimo kama matrekta wanaweza kuazima kwenye chama.
Kwa upande wake katibu wa (UVCCM) Kibaha Mjini David Malecela alisema kuwa wana maeneo mengi ambayo hata hivyo hayajaendelezwa hali ambayo imesababisha watu kuyavamia.
Malecela alisema kuwa kwa sasa wako kwenye mipango ya kuhakikisha wanayamiliki kisheria ili kukabiliana na watu wanaoyavamia maeneo yao ambayo yakiendelezwa yatakuwa ni moja ya vyanzo vikuu vya mapato ya umoja.
Mwisho.

WAPEWA SIKU 60 KUHAMA ENEO LILILOFUTIWA HATI YA UMILIKI

Na John Gagarini, Kibaha
BAADHI ya wakazi wa Kitongoji cha Vinziko Kijiji cha Kikongo wilayani Kibaha mkoani Pwani wameitaka Halmashauri ya wilaya kutowaondoa kwenye eneo ambalo wanaishi kwani hawana pa kwenda.
Serikali iliwapa siku 60 wawe wameondoka kwenye eneo hilo ambalo lilikuwa chini ya kampuni ya United Framing Cooperation (UFC) ambao walishindwa kuliendesha na kuwa shamba pori kabla ya serikali haijalifutia hati Mei 28 mwaka 2015.
Moja ya wakazi wa eneo hilo Athuman Fundi (90) alisema kuwa wao wako hapo muda mrefu tangu operesheni vijiji ambapo walihamishwa toka maeneo ya mbali na kupelekwa maeneo ambayo yalikuwa karibu na huduma za kijamii.
“Sisi tulifikiri ni vema wakatuacha kwenye maeneo yetu haya na si kutuondoa kwani hatuna pa kwenda na sisi hapa tumeshawekeza kwa kujenga makazi ya kudumu leo wakituambia tuondoke tutakwenda wapi vinginevyo watulipe ili tukatafute sehemu nyingine au watupatie maeneo mengine,” alisema Fundi.
Fundi alisema kuwa mbali ya kutakiwa kuondoka pia vyombo vya dola vimekuwa vikitumia nguvu kubwa kutaka wao waondoke ambapo wenzao wamekuwa wakikamatwa kutokana na mgogoro huo ambao umewanyima raha.
“Tunaomba tusaidiwe na Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi ili tupate haki yetu kwani wao kututaka tuondoke bila ya kutupa chochote au kutotupa maeneo mengine tunaona kama hatujatendewa haki kwani tuna nyumba zetu, mazao ambavyo vimo humo leo wanatuambia tuviondoe tutaishi wapi,” alisema Fundi.
Kwa upande wake Sabina Benedict alisema kuwa wamekuwa wakiteseka sana kutokana na mgogoro huo kwani wazee na vijana wamekuwa wakikamatwa na polisi na kuwekwa rumande hivyo kuishi kwa woga.
Benedict alisema kuwa tatizo kubwa linatokana na viongozi ambao wanataka kumuuzia mwekezaji ambaye anatumia kila njia kuhakikisha wao wanaondoka ili alipate eneo hilo kirahisi.
Naye mwenyekiti wa Kijiji cha Kikongo Sultan Ngandi alisema kuwa shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 3,285 lilikuwa likimilikiwa na kampuni hiyo ya UFC ambayo ilikuwa ikilima mazao mbalimbali kama vile Pamba, Mbaazi, Alizeti na mazao mengine ilishindwa kuliendeleza na kuliacha pori ambalo lilikuwa likitumiwa na wahalifu kuzuru watu.
Ngandi alisema kuwa wananchi waliomba kulima ikiwa ni pamoja na Umoja wa wakulima wa Ondoa Njaa Kikongo (ONJAKI) lakini walitakiwa wasilime mazao ya kudumu wala kujenga nyumba za kudumu badala yake walime mazao ya muda mfupi.
“Hata hivyo baadhi ya watu walikiuka makubaliano na wengine walianza kujenga nyumba za kudumu, mazao ya muda mrefu na hata wengine walifikia hatua ya kuayauza kienyeji baadhi ya maeneo nao kuondoka na kuwaacha watu ambao ndiyo wanaolalamika,” aisema Ngandi.
Akizungumzia suala hilo mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba alisema kuwa ni kweli wametoa siku 60 kwa watu walioko kwenye eneo hilo kwani wamevamia na hawakutakiwa kuwa kwenye neo hilo kwani liko chini ya serikali.
Kihemba alisema kuwa hilo ni moja ya mashamba 16 ambayo yalifutiwa hati na kwa sasa wanaendelea na mchakato wa kulitengea matumizi na waliwataka watu walioko kwenye eneo hilo wapeleke vielelezo vya kuonyesha walipataje maeneo hayo na kusema si kweli kwamba kuna mwekezaji wanataka kumpa eneo hilo.
Aidha alisema kuwa hadi sasa watu zaidi ya 100 wamepeleka vielelezo vyao nab ado wanawasubiri watu wengine ambao wako wengi ili wapeleke vielelezo vyao ili serikali iangalie namna ya kuwasaidia na kuwataka watu hao waondoke kwenye eneo hilo.
Mwisho.

Friday, April 1, 2016

SAKATA WAFANYAKAZI HEWA RC AWATAKA WAKURUGENZI KUBAINISHA WALIOKUWA WAKICHUKUA MISHAHARA PASIPO KUWA WAFANYAKAZI

Na John Gagarini, Kibaha
SAKATA la wafanyakazi hewa mkoani Pwani limeingia hatua mpya baada ya Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa huo kutakiwa kutoa taarifa zaidi juu ya wafanyakazi hewa 42 ambao hawapo kabisa kazini lakini wamekuwa wakipokea mishahara kila mwezi.
Jumla ya wafanyakazi 42 kwenye mkoa huo majina yao yapo lakini wao hawapo kazini lakini walikuwa wakipokea mishahara kila mwezi hali ambayo imeisababishia hasara kubwa serikali kutokana na kulipa hewa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kiwake mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa wafanyakazi hao hewa wamewekwa kwenye madaraja mbalimbali ikiwa ni pamoja na hao 42 ambao hawapo kabisa kazini lakini walikuwa wanalipwa.
“Kutokana na hali hii nimewapa wakurugenzi hadi siku ya Jumatano Aprili 6 wawe wameniletea taarifa juu ya watu waliokuwa wakipokea fedha hizo kwani haiwezekani ni nani aliyekuwa akipokea fedha hizo licha ya kutokuwepo kabisa kwa wafanyakazi hao,” alisema Ndikilo.
Ndikilo alisema kuwa haiwezekani fedha zilipwe kwa wafanayakazi ambao hawapo kazini kwani ni jambo la kushangaza na lazima ajulikane ambaye alikuwa akipokea fedha hizo kwani kundi hili ni hewa kabisa.
“Kundi lingine ni la wafanyakazi 58 ambao wamesimamishwa kazi kwa tuhuma mbalimbali lakini wamekuwa wakipokea mishahara kama kawaida tunataka tujuea kwa undani ni tuhuma gani zinazowakabili na hatua zilizochukuliwa dhidi yao,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa kundi lingine ni la wafanyakazi ambao wako kazini lakini ni watoro hawaendi kazini lakini mishahara wanachukua kama kawaida licha ya kwamba hawawajibiki kazini kama ilivyo taratibu za utumishi wa umma.
“Tunataka kila mkurugenzi atoe taarifa sahihi bila ya kuficha kwani endapo atabainika ameficha taarifa hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake hivyo ni vema wakawea wazi taarifa za hao wafanyakazi hewa,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa juu ya hasara waliyoiingiza wafanyakazi hao hewa ambapo kwa mkoa wa Pwani ni 150 bado wanaendelea na uchunguzi ili kubaini ni kiasi gani ambacho wameliingizia Taifa hasara na mara watakapokamilisha watatoa taarifa hizo.

Mwisho.

SELEMAN TALL ATWAA MKANDA WA TPBO

Na John Gagarini, Kibaha
BONDIA Said Seleman maarufu kama Tall juzi usiku alitwaa ubingwa wa taifa wa ngumi uzito wa kati kupitia shirikisho la ngumi la TPBO baada ya kumshinda kwa pointi Ambokile Chusa.
Pambano hilo ambalo lilipigwa kwenye ukumbi wa Container wilayani Kibaha mkoani Pwani lilikuwa la vuta ni kuvute kutokana na umahiri wa mabondia hao ambao hata hivyo walikuwa wakicheza kwa kuogopana kwa hofu ya kupoteza ushindi.
Hata hivyo Tall alikuwa mjanja na kumzidi mbinu mpinzani wake ambaye muda mwingi alikuwa akijihami kwa kuficha uso ili kukwepa ngumi kali zilizokuwa zikirushwa na mpinzani wake.
Kwenye mapambano mengine Yasini Said alimpiga Julius Jackson, Emanuel Endrew alimpiga Ramadhan Keshi, Ramadhan Kamage alimtwanga Kassim Chuma, Salehe Muntari alimtwanga Aziz Pendeza, Hassan Mgosi alimtwanga Hemed Hemed, Said Chino alimtwanga Idd Mgwinyo kwa TKO, huku Alfred Masinda na Nurdin Mijibwa na Abdala Luwanje na Rajabu Mbena walitoka sare.
Akikabidhi mkanda huo kutoka TPBO mgeni rasmi katika pambano hilo Selina Wilson Diwani wa Viti Maalumu aliwapongeza waandaaji wa pambano hilo Butamanya Promotion kwa kuleta shindano hilo Kibaha.
Wilson alisema kuwa kuleta mchezo huo Kibaha ni kuibua vipaji vilivyopo mikoani na kuwapa uzoefu mabondia wa hapa kuweza kujifunza mbinu za ngumi.
“Mimi ni kijana na nimeona jinsi gani watu wanavyopenda mchezo huu hapa Kibaha na mkoa wa Pwani nitahakikisha naunga mkono mchezo huu na kupeleka halamashauri changamoto zinazowakabili ili ziweze kufanyiwa kazi kwa lengo la kuboresha mchezo huu,” alisema Wilson.
Kwa upande wake bondia wa zamani Habibu Kinyogoli alisema kuwa mabondia wa mkoa wa Pwani wameonyesha uwezo lakini walichokosa ni mbinu za mapigano hivyo atajitolea kuwafundisha mabondia wa mkoa wa Pwani.

Mwisho.