Na John Gagarini, Kibaha
SAKATA la wafanyakazi hewa mkoani Pwani limeingia hatua mpya
baada ya Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa huo kutakiwa kutoa taarifa zaidi
juu ya wafanyakazi hewa 42 ambao hawapo kabisa kazini lakini wamekuwa wakipokea
mishahara kila mwezi.
Jumla ya wafanyakazi 42 kwenye mkoa huo majina yao yapo
lakini wao hawapo kazini lakini walikuwa wakipokea mishahara kila mwezi hali
ambayo imeisababishia hasara kubwa serikali kutokana na kulipa hewa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kiwake mkuu
wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa wafanyakazi hao hewa
wamewekwa kwenye madaraja mbalimbali ikiwa ni pamoja na hao 42 ambao hawapo
kabisa kazini lakini walikuwa wanalipwa.
“Kutokana na hali hii nimewapa wakurugenzi hadi siku ya Jumatano
Aprili 6 wawe wameniletea taarifa juu ya watu waliokuwa wakipokea fedha hizo
kwani haiwezekani ni nani aliyekuwa akipokea fedha hizo licha ya kutokuwepo
kabisa kwa wafanyakazi hao,” alisema Ndikilo.
Ndikilo alisema kuwa haiwezekani fedha zilipwe kwa
wafanayakazi ambao hawapo kazini kwani ni jambo la kushangaza na lazima
ajulikane ambaye alikuwa akipokea fedha hizo kwani kundi hili ni hewa kabisa.
“Kundi lingine ni la wafanyakazi 58 ambao wamesimamishwa kazi
kwa tuhuma mbalimbali lakini wamekuwa wakipokea mishahara kama kawaida tunataka
tujuea kwa undani ni tuhuma gani zinazowakabili na hatua zilizochukuliwa dhidi
yao,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa kundi lingine ni la wafanyakazi ambao wako
kazini lakini ni watoro hawaendi kazini lakini mishahara wanachukua kama
kawaida licha ya kwamba hawawajibiki kazini kama ilivyo taratibu za utumishi wa
umma.
“Tunataka kila mkurugenzi atoe taarifa sahihi bila ya kuficha
kwani endapo atabainika ameficha taarifa hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa
dhidi yake hivyo ni vema wakawea wazi taarifa za hao wafanyakazi hewa,” alisema
Ndikilo.
Aidha alisema kuwa juu ya hasara waliyoiingiza wafanyakazi
hao hewa ambapo kwa mkoa wa Pwani ni 150 bado wanaendelea na uchunguzi ili
kubaini ni kiasi gani ambacho wameliingizia Taifa hasara na mara
watakapokamilisha watatoa taarifa hizo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment